Michezo

Transfoc mbioni kulipiza kisasi

April 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

PATASHIKA saba zimepangwa kuchezwa wikendi hii kwenye mfululizo wa mechi za Kundi B Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza msimu huu. 

Transfoc FC itakuwa katika ardhi ya nyumbani kukaribisha Kisumu Hotstars katika Uwanja wa Kenyatta Stadium mjini humo.

Transfoc ya kocha, Peter Olukusa itateremka dimbani ikiumiza majeraha ya kupigwa bao 1-0 na Maafande wa APs Bomet wiki iliyopita. Katika mpango mzima wachezaji hao watakuwa kazini kuwinda ushindi kulipiza kisasi baada ya kupoteza mechi mbili mflululizo.

”Hata tunashindwa kuelewa mbona vijana wetu wanalegeza kamba kwenye mbio za msimu huu lakini tunatumai hali itakuwa sawa,” alisema meneja wa Transfoc, Pascal Wekesa na kuongeza kwamba kampeni za msimu huu kamwe siyo rahisi.

Transfoc imejikuta njia panda kwenye mbio hizo ambapo imeteremka na kutua nafasi ya saba kwa kufikisha alama 19 , mbili mbele ya Transmara Sugar FC inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza.

Nao wachana nyavu wa Zoo Youth wanaofunga tatu bora kwa alama 27 watakuwa ugenini kukabili Muhoroni Youth ya 11 kwenye jedwali kwa kuzoa alama 15.

Nayo Vihiga Bullets ambayo hutiwa makali na kocha, Edward Manoah kati ya vikosi vinavyotisha kwenye kampeni hizo, Jumapili itazuru mjini Eldoret kumenyana na G.F.E 105 FC.

Kwenye ratiba hiyo, Transmara Sugar itakutanishwa na Raiply FC, Silibwet itachuana na Bondo United, nayo Poror Mote itakwaruzana na St Josephs Youth Academy.