Makala

Transfoma ya polo nusra ing’olewe na mbwa akijisaidia kwenye shamba usiku

February 25th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

JOMBI mmoja katika Kaunti ya Nyeri anauguza majeraha ya sehemu za nyeti baada ya kuvamiwa na mbwa akijisaidia haja kubwa kwenye shamba la wenyewe. 

Kwa mujibu wa mdokezi, kalameni alikuwa akielekea nyumbani kutoka baa mwendo wa saa sita usiku alipohisi msukumo wa haja kubwa.

“Jamaa aliingia kwa shamba lililokuwa karibu na akaanza harakati za kujipa afueni. Labda sauti za hewa na haja yake zikimtoka ndizo zilimuuza kwa mbwa wa boma hilo ambao walimpata akiwa amejikunyata kwa mimea ya mahindi akishiriki misukumo yake ya kutoa uchafu mwilini,” mdaku wetu akaeleza.

Katika haraka yake ya kusaka afueni ya tumbo lake, hakuzingatia mikakati ya kiusalama katika maboma ya watu ila tu aliruka kwa shamba ambalo mbwa wa ulinzi walikuwa wakingojea kazi.

Mbwa hao walikuwa watatu na walimvamia na kumshambulia kama adui mvamizi wa himaya yao.

“Pombe ilimwishia kwa kichwa na akapiga nduru ajabu. Hali hiyo ya makelele ya polo akiraruliwa nao mbwa wakibweka na kunguruma ziliwaamsha wenye boma ambao kufika eneo la mkasa walimpata jombi akiwa hana nguo,” akasema mdokezi.

Baada ya kuhojiwa na kubainika kwamba hakuwa mhalifu wa wizi bali wa mazingira, alifanyiwa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika hospitali ya Karatina.

“Alikuwa amechezewa vilivyo kwa meno makalioni na hata kwa nyeti zenyewe. Tunamuombea Mungu apone na nguvu zake za kiume zisiwe ziliadhirika,” akasema rafiki wa jombi huyo.

 

[email protected]