Makala

Trekta ndogo kivutio cha vijana kushiriki kilimo 

March 20th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MATUMIZI ya mitambo, mashine na teknolojia za kisasa yanatajwa kama mojawapo ya mbinu kuboresha shughuli za kilimo.

Kimsingi, mfumo huo unarahisisha shughuli shambani, kando na kusifiwa kusaidia kuongeza mzao.

Huku idadi ya vijana wanaoshiriki zaraa ikiwa ingali chini, teknolojia za kileo wadau katika sekta ya kilimo wanasema ni njia maalum kuwavutia.

Nyabon Enterprises Ltd, kampuni inayounda mseto wa mashine inaangazia gapu hii.

Ikiwa na makao yake Kisumu, kwenye mtandao wake wa mashine, Vincent Odhiambo, Meneja wa Soko na Mauzo, anasema ina trekta ndogo ambazo ni kivutio cha vijana.

“Wanakwepa kilimo kwa sababu wanataka teknolojia zenye mvuto,” Odhiambo anasema.

Mfano, trekta yenye nguvukawi 27HP Compact ya injini ya silinda-4, afisa huyu anaisifia kuwa bora kufanya kilimo kwenye mashamba madogo.

Trekta ndogo yenye nguvukawi 27HP. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kwa sababu ya upungufu wa mashamba, yaliyopo yakiwa madogo, wanahitaji kivutio cha kuendeleza kilimo kwa kutumia mashine zinazoingiana na kiwango kilichopo. 27HP Compact Mini Tractor, ina uwezo kulima ekari 5 tano kwa siku, kila ekari ikitumia wastani wa lita tano za mafuta ya dizeli,” anaelezea.

Mbinu za kitambo kuendeleza kilimo, hasa matumizi ya mafahali, zinachosha, hatua ambayo inafisha nyoyo za vijana kushiriki katika mtandao wa uzalishaji chakula.

“Tukikumbatia matumizi ya bunifu na teknolojia za kisasa, vijana watatekwa na kiwango cha uzalishaji chakula Kenya kitaongezeka mara dufu. Isitoshe, ni mojawapo ya njia kubuni nafasi za ajira,” anasema mtaalamu wa masuala ya kilimo Esta Kamau.

Wakulima wakijionea trekta ndogo katika maonyesho ya ASK. PICHA|SAMMY WAWERU

Bi Esther amewahi kuhudumu kama Meneja wa Heifer International tawi la Kenya, shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalopiga jeki wakulima nchini kunogesha uzalishaji wa chakula.

Aidha, Heifer ina mpango maalum kusaidia wakulima kumiliki trekta unaojulikana kama Mechanization for Africa.

Moango huo uliozinduliwa miaka mitatu iliyopita, unaendelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya Hello Tractor.

“Matumizi ya trekta ni mojawapo ya mbinu kurahisisha shughuli za kilimo na kuvutia vijana wajiunge na sekta ya kilimo kusaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji,” anasema Adesuwa Ifedi, Naibu Rais Heifer International.

Nchi zilizoimarika kiuzalishaji, zinaendelea kuibuka na mifumo na teknolojia mpya kuvutia vijana katika kilimo.


Jembe la trekta ya mashamba madogo. PICHA|SAMMY WAWERU