Habari za Kaunti

Treni za abiria zasitisha uchukuzi jijini kufuatia mvua kubwa

April 24th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Reli Nchini (KRC) limesitisha huduma za uchukuzi wa umma jijini Nairobi kufuatia mvua kubwa ambayo imesababisha mafuriko katika maeneo kadhaa nchini.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, shirika hilo lilisema kuwa mafuriko yameathiri reli na hivyo ni vigumu kwa treni kuhudumu.

“Shirika la Reli Nchini lingependa kujulisha umma kwamba limesitisha kwa muda safari za treni kati ya mitaa mbalimbali na katikati mwa jiji. Hii ni kwa sababu mafuriko yameharibu udongo ulioko kando ya reli na hivyo ni vigumu kwa treni kuhudumu,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo ya KRC.

Treni hizo huhudumu kati ya katikati mwa jiji na maeneo ya Syokimau, Dandora, Ruiru, Pipeline miongoni mwa vituo vingine.

Shirika la KRC halikusema lolote kuhusu safari zake za ruti za maeneo mbalimbali kama vile kutoka Nairobi kwenda Mombasa, Kisumu na Nanyuki.