Kimataifa

Trump aashiria kutong’atuka akishindwa uchaguzini ujao

July 20th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

RAIS Donald Trump wa Amerika amedokeza kwamba hana mpango wa kung’atuka mamlakani baada ya uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika nchini humo mnamo Novemba mwaka huu.

Akiulizwa ikiwa atakubali matokeo ya uchaguzi huo endapo atashindwa, Trump alirudia msimamo wake wa 2016, akisema, “Nitaona… sitasema ndiyo nimeshindwa.”

Mahojiano hayo ambayo yalinakiliwa mapema, yanajiri wakati ambapo matokeo ya kura ya maoni ya hivi punde yanaonyesha kuimarika kwa umaarufu wa mgombeaji wa chama cha Democrat Joe Biden huku tashwishi ikitanda nchini humo kuhusu namna Rais Trump anashughulikia janga la Covid-19 nayo maambukizi yakiongezeka katika majimbo mengi.

Chris Wallace aliyeendesha mahojiano hayo alimwambia Rais Trump kwamba matokeo ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na Shirika la habari la Fox News linaonyesha kuwa Waamerika wengi wanaamini kuwa Biden ana uwezo sio tu wa kushughulikia Covid-19 bali hata uchumi wa Amerika.

Trump amekuwa akijinadi kama kiongozi ambaye anaweza kufufua uchumi wa Amerika ulioathirika pakubwa na janga la corona.

Na matokeo mengine ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na mashirika ya habari ya Washington Post na ABC News, kwa pamoja, yanaonyesha Biden akiongoza Trump katika umaarufu miongoni mwa wapigakura waliosajiliwa kote nchini Amerika. Biden anaungwa mkono na asilimia 55 ya wapigakura huku Trump akiungwa na asilimia 40 ya wapigakura.

Trump alipuuzilia mbali matokeo hayo akiyataja kama “feki” akisema tafiti zilizoendeshwa na Ikulu ya White House zinaonyesha kuwa yeye ni maarufu zaidi kitaifa na katika majimbo yenye idadi kubwa ya wapigakura na ambayo huamua mshindi katika chaguzi za urais.

Alimshambulia Biden mara kadha akisema kuwa “hajahitimu” kuongoza Amerika. Biden huwa haonekani kwenye majukwaa ya kampeni kutokana na marufuku yaliyowekwa kutokana na janga Covid-19.

“Hana uwezo kimwili na kiakili,” Trump akasema akimrejelea Biden kwenye mahojiano na “Fox News Sunday”.

Huku Trump mwenye umri wa miaka 74 alihoji uwezo wa mshindani kiakili, Wallace alimuuliza ikiwa anaamini kuwa Biden mwenye umri wa miaka 77, umelemewa na uzee.

“Sitaki kusema hivyo,” Trump akajibu, “Nasema kuwa hana sifa za kumwezesha kuwa rais.”

Trump alisema Biden ambaye ni makamu wa rais wa zamani hawezi kujibu maswali magumu kuhusu masuala ya uongozi kwa sababu uwezo wake wa kukumbuka dhana mbalimbali umeshuka zaidi.

“Biden hawezi kustahimili mahojiano kama haya. Atazirai na kuomba apelekwe nyumbani,” Trump akasema.

Kulingana na Rais huyo, endapo Biden atachaguliwa katika uchaguzi mnamo Novemba 3, “ataharibu Amerika.”

Rais huyo ambaye anakabiliwa na changamoto kama vile janga la Covid-19, maandamano dhidi ya dhuluma za ubaguzi dhidi ya Waamerika weusi na kudhoofika kwa uchumi, alidai bila ithibati, kuwa Biden ataongeza ushuru na kuvunja polisi endapo atachaguliwa kuwa rais.