Kimataifa

Trump adai alizimiwa mtandao asihojiwe na bilionea Elon Musk

Na MASHIRIKA August 13th, 2024 2 min read

WASHINGTON D.C, AMERIKA

MAHOJIANO kati ya aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump na mmliki wa mtandao wa X, Elon Musk yalikumbwa na mushkili wa mitandao na ukaanza dakika 40 baada ya muda uliopangwa Jumatatu usiku.

Amerika ni kati ya nchi kubwa zenye mitandao thabiti ila kulikuwa na hitilafu si chache kabla ya Trump kuhojiwa na bwanyenye huyo mmiliki wa X (zamani Twitter).

Haya yalikuwa mahojiano ya kwanza kwa Trump tangu apigwe marufuku na X mnamo Januari 6, 2021 alipotuhumiwa kuchangia katika maandamano yaliyofuata ushinde wake kwenye uchaguzi.

Musk alimrejeshea akaunti yake ya X mwaka mmoja uliopita lakini kiongozi huyo hajawa akipachika hotuba zake katika mtandao huo, ikilinganishwa na zamani ambapo alipenda sana kuutumia. Trump ndiye mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Truth Social aliobuni baada ya kupigwa marufuku na Twitter.

Wengi wa watumizi wa mitandao walitatizika kupenya na kuyafuatilia mahojiano hayo yaliyokuwa yakipeperushwa moja kwa moja mtandaoni.

Musk aliwalaumu wadukuzi wa mitandao kwa kujaribu kuteka jukwaa la X ambako mahojiano hayo yalikuwa yakiendelea.

Mtaalamu wa Masuala ya Teknolojia Andrew Hay alisema huenda tatizo hilo lilitokana na njama ya wadukuzi wa mitandao waliolenga kuyavuruga mahojiano hayo.

“Ninashuku wengi walikuwa wakijaribu kuingia na kufuatilia lakini kwa sababu pia ni wakati wa siasa huwezi kupuuza kabisa suala linaloibuliwa la udukuzi,” akasema Hay.

Hata hivyo, Trump si mwaniaji wa kwanza wa urais kukabiliwa na tatizo hilo. Mnamo Mei 2023, Gavana wa Florida Ron DeSantis, aliyekuwa akizindua kampeni ya kuwania urais kupitia X hakufanikiwa kutokana na mtandao huo kuingiliwa na wadukuzi.

Trump atakuwa akilenga sasa kutumia X kujipigia debe kwa raia akilenga kuwahi urais na kuhudumu muhula wake wa mwisho.

Tayari mtandao wake wa X una mabango mengi yanayomsawiri kama kiongozi mwokozi wa Amerika japo mikutano yake ya kampeni haijakuwa ikiangaziwa sana humo.

Mahojiano kati ya Musk na Trump yalikuwa ya marafiki na aliulizwa maswali rahisi na mmiliki huyo wa X.

Japo wawili hao walikuwa mahasimu zamani, sasa ni marafiki baada ya Musk kuweka hadharani kuwa anaunga mkono mwaniaji huyo wa chama cha Republican.

Trump anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mwaniaji wa Democratic na Makamu wa Rais Kamala Harris baada ya Rais Joe Biden kujiondoa kwenye kiny’ang’anyiro hicho mwezi jana.

“Amerika itakuwa mahali pazuri mikononi mwako na utamshinda Kamala,” Musk akamwambia Trump wakati wa mahojiano hayo.

Mada nyingine ambayo wawili hao walizungumzia ni jaribio la kumuua Trump katika mkutano wa kisiasa mwezi uliopita Pennesylvania.
Pia waliongea kuhusu masuala ya uhamiaji na usalama wa nchi hiyo.

Trump mwenyewe alijipigia debe na kuahidi kuondoa baadhi ya sera za Rais Biden ambazo alisema zimeiweka nchi hiyo katika hatari ya kushambuliwa na maadui mbali na kuwaumiza pia raia asili wa taifa hilo.