Habari

Trump aiga Raila

November 6th, 2020 3 min read

Na MWANDISHI WETU

VIOJA, ubishi na taharuki ambazo zimeshuhudiwa Amerika wakati wa uchaguzi wa mwaka huu 2020 zimeibua mjadala mkali hapa Kenya, wengi wakifananisha hatua za Rais Donald Trump na zile za Kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo 2017.

Mnamo Jumatano wakati Trump alijitokeza kupinga matokeo ya uchaguzi kabla hesabu zikamilike, Wakenya katika mitandao ya kijamii walikuwa tayari wameanza kusambaza taarifa, picha na video ambazo zilimfananisha na Bw Odinga hasa alipokuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa 2017.

Trump alikuwa akilalamika akidai kuna hujuma katika mbinu za kuhesabu kura kwani aliamini mpinzani wake Joe Biden wa chama cha Democratic alikuwa anapendelewa.

Katika mojawapo ya taarifa, Trump alidai Biden ‘anajaziwa’ kura kwa njia za ‘kimiujiza’ kusudi aibuke mshindi.

“Jana usiku nilikuwa ninaongoza kwa idadi kubwa ya kura katika majimbo mengi muhimu kisha ghafla, moja moja, zikaanza kupotea kimiujiza,” akadai Trump.

Katika uchaguzi wa 2017 hapa Kenya, Bw Odinga alilalamika kwamba kura za Rais Uhuru Kenyatta zilikuwa zinaongezeka kwa njia isiyoeleweka.

Wanachama wa ODM wakati huo walidai mbinu za kitekinolojia zilitumiwa kuhakikisha kura za Jubilee ziliongezeka kwa kiwango mahsusi zaidi kuliko za ODM hadi Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wakatangazwa washindi.

Lakini kwa Trump, wizi wa kura aliolalamikia bila kutoa ushahidi wowote, ulidaiwa kutendeka kutoka kwa kura zilizotumwa kupitia posta.

“Wanapata kura za Biden kila mahali; hii ni hatari kwa nchi,” akasema Trump.

Mamilioni ya Waamerika walikuwa wametuma kura zao mapema kwa njia ya posta jinsi inavyokubaliwa kisheria nchini humo, lakini zilikuwa zingali zinahesabiwa kufikia Alhamisi.

Nyingi ya kura zilizotumwa kwa posta zilionekana kuegemea upande wa Biden.

Idadi ya waliotuma kura kwa posta iliongezeka mwaka huu kwa sababu ya janga la corona ambalo lilifanya wengi kuepuka kupiga foleni siku ya uchaguzi.

Malalamishi kuhusu wizi wa kura yalifanya wafuasi wa Trump kumiminika barabarani katika majimbo tofauti kwa maandamano, huku uharibifu ukishuhudiwa katika baadhi ya maeneo. Polisi waliwakamata waandamanaji kadhaa waliosemekana kuvuruga amani.

Hali hii haikuwa tofauti na jinsi ilivyokuwa nchini wakati wafuasi wa Bw Odinga walipoamini kulikuwa na wizi wa kura uchaguzini na wakaandamana hasa Kisumu na Nairobi.

Mashirika ya habari Amerika yalieleza kuwa baadhi ya waandamanaji nchini humo tangu Jumatano walikuwa na silaha kama vile bunduki ambazo ni rahisi kwa raia kumiliki kisheria.

Wakati hayo yakiendelea, maafisa wanaosimamia kampeni ya Trump katika baadhi ya majimbo waliamua kuelekea mahakamani kutaka kura zihesabiwe upya.

Wanataka kura zihesabiwe upya katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania, ambayo huwa muhimu kwa mgombeaji yeyote wa urais Amerika.

Hii ni baada ya Trump kuapa kuwa ataelekea katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo endapo Biden atatangazwa mshindi.

Hatua hii ilifananishwa na jinsi Bw Odinga alivyoamua kuelekea mahakamani baada ya chaguzi za 2013 na 2017.

Katika mwaka wa 2013, Mahakama ya Juu ilishikilia kwamba hapakuwa na dosari uchaguzini lakini katika mwaka wa 2017, mahakama hiyo inayosimamiwa na Jaji Mkuu David Maraga ikaweka historia kwa kufutilia mbali matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Odinga na wenzake katika Muungano wa National Super Alliance (NASA) walikataa kushiriki marudio ya uchaguzi mnamo Oktoba 26 mwaka huo, wakisisitiza mabadiliko yalitakikana kwanza katika IEBC.

Ni hatua hii iliyomsukuma Bw Odinga kujitangaza ‘rais wa wananchi’ mwaka wa 2018 alipoapishwa na wandani wake wakiwemo Mbunge wa Ruaraka, T.J Kajwang na wakili Miguna Miguna aliyefurushwa nchini baadaye.

Wakenya katika mitandao ya kijamii jana walikuwa wanaendeleza wito wa kumtaka Trump afuate nyayo za Bw Odinga endapo anaamini uchaguzi haukuwa wa haki.

Akizungumzia suala hilo, Bw Miguna alitania kwamba yuko tayari kumwapisha Trump kuwa ‘rais wa wananchi’ jinsi alivyomwapisha kiongozi wa ODM.

“Kwa Donald Trump: Mimi ni wakili aliyehitimu jijini Ontario, Canada. Nimepokea maagizo kutoka kwa mamilioni ya Wakenya walioniomba nikuapishe kuwa ‘rais wa wananchi’. Tafadhali wasiliana nami ili tujadiliane kuhusu ada zangu na mahitaji mengine,” Bw Miguna akamwambia Trump katika mtandao wa Twitter.

Sawa na Bw Odinga, Trump alidai maajenti wake walizuiliwa kufuatilia jinsi hesabu za kura zinafanywa katika baadhi ya vituo.

Kufikia wakati wetu kuchapisha gazeti, matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais Amerika yalikuwa hayajatangazwa.