Kimataifa

Trump akana kuwahi kusema Clinton afungwe jela

June 3rd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

ALIYEKUWA Rais wa Amerika, Donald Trump alidai Jumapili kwamba hakutaka aliyekuwa mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2016, Hillary Clinton, afungwe.

Trump alisema hayo wakati wa mahojiano na shirila la habari la Fox News akisema: “Sikusema afungiwe jela.”

Trump, ambaye anakabiliwa na kesi ambayo ina uwezekano mkubwa wa kumfunga — baada ya kuwa rais wa kwanza wa Amerika kuhukumiwa kwa tetesi za uhalifu, alipendekeza mara kwa mara Clinton kufungwa jela wakati wakiwa wanapambana katika kampeni za urais 2016.

Makelele na wimbo wa “mfungie” yaliwaudhi wafuasi wake kwenye mikutano yake wakati wa kampeni na kwa miaka kadhaa baadaye, na alisema kwamba alikubaliana na matamshi ya ‘mfungie’ na pia kuomba Clinton kufungwa jela katika mikutano mingi.

Wakati wa mahojiano hayo yaliyopeperushwa Jumapili, mtangazaji wa Fox, Will Cain alihoji Bw Trump, aliye na umri wa miaka 77 kuhusu hisia zake, ambazo zilihusu matumizi ya Clinton ya seva ya barua pepe ya kibinafsi alipokuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika wakati huo.

“Ulisema kwa kusisitiza, kuhusu Hillary Clinton, ‘Afungiwe jela.’ Ulikataa kufanya hivyo kama rais,” Cain alisema.

“Nilimshinda,” Trump alijibu. “Ni rahisi ukiwa umeshinda kiti. Na kila mara walisema ‘mfungieni jela,’ na nilihisi — na ningeweza kufanya hivyo, lakini nilihisi lingekuwa jambo baya sana. Na kisha hili lilinitokea. Na hivyo ninaweza kuhisi tofauti juu yake.”

Aliendelea kukataa kujihusisha na kuhusika moja kwa moja na kauli hiyo.

“Sikusema ‘mfungieni jela,’ lakini watu walisema afungwe, afungwe,” Trump alisema.

“Kisha, tulishinda. Na ninasema- na nilisema, ndio kwa uwazi, tulia, tutembee pamoja. Tuna nchi tunayostahili kuipa kipaumbele kuijenga.”

Bi Clinton, mke wa aliyekuwa rais wa Amerika Bill Clinton alichunguzwa kuhusu seva ya baruapepe aliyotumia kibinafsi.

Hata hivyo, hakupatikana na hatia.

Wiki jana, Trump alishtakiwa kwa makosa 34 kuwa na stakabadhi ghushi za biashara ili kufunika ukweli kuhusu malipo kwa mchezaji sinema za ngono maarufu mwaka 2016.

Tarehe yake ya kuhukumiwa kortini itakuwa Julai 11 mwaka huu.

Katika mahojiano hayo pia, Trump alikiri kwamba anaweza kufungwa jela, akionya kwamba ingawa atakubaliana na hukumu atakayopewa, hatua kama hiyo itawavunja moyo wafuasi wake.

Onyo hilo limetokea katika nchi ambayo tayari ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea kwa ghasia za kisiasa katika kipindi hiki wanapoelekea katika uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 5 mwaka huu.