Kimataifa

Trump akiri kuambukizwa corona kumemtatiza sana

October 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON DC, Amerika

RAIS wa Amerika Donald Trump ambaye amelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa virusi vya corona, amekiri kwamba kuambukizwa virusi hivyo kunampatia wakati mgumu na ni mtihani kwake.

Ingawa madaktari wake wanasema anaendelea vyema, Trump alisema kwamba siku chache zijazo zitakuwa mtihani halisi kwake.

Rais huyo alichapisha video kwenye mtandao wa Twitter siku ya pili akiwa hospitalini anakotibiwa Covid-19 kueleza masaibu yake baada ya ripoti za kukanganya kutolewa.

Katika video hiyo, Trump anawashukuru madaktari na wauguzi katika hospitali ya kijeshi ya Walter Reed National Military Medical Center jijini Washington DC anakotibiwa.

“Nilikuja hapa, sikuwa nikihisi vyema sana. Sasa nimepata afueni,” alisema na kuongeza: “Kwa siku chache zijazo, ninaamini utakuwa mtihani halisi. Tutaona kitakachotendeka katika muda wa siku chache zijazo.”

Alisema anataka kurudi kwa kampeni yake ya uchaguzi.

“Nitarudi, ninafikiri nitarudi karibuni. Ninataka kukamilisha kampeni nilivyoanza,” alisema.

“Tutashinda virusi hivi vya corona au vile mnavyopenda kuviita, na tutashinda sawasawa.”

Mnamo Jumamosi, daktari wake alisema Trump alikuwa amepata afueni lakini hakuwa amepona. Kulikuwa na ripoti za kukaganya kuhusu hali ya afya yake.

Muda mfupi baada ya madaktari wake kutoa taarifa yao, mkuu wa wafanyakazi wa Ikulu ya White House, Mark Meadows, alisema kwamba hali ya afya ya Rais huyo ilitia wasiwasi.

Duru zilisema kwamba Trump hakufurahishwa na kauli ya Meadows.

Mke wa Trump na washirika wa karibu wa rais huyo pia wameambukizwa corona. Wengi wao walihudhuria hafla waliyosongamana katika White House ambapo Trump alimteua Amy Coney Barret kuwa jaji wa Mahakama ya Juu. Inashukiwa watu wengi waliambukizwa corona kwenye hafla hiyo.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Amerika, mshirika wa Trump kuambukizwa hivi punde ni Nicholas Luna.

Mnamo Jumamosi madaktari walisema kwamba Trump hakuwa ameongezwa oksijeni kumsaidia kupumua na kwamba hakuwa na joto katika muda wa saa 24.

Lakini kauli ya Mark Meadows kwa wanahabari ilitoa taswira tofauti.

“Hali ya Rais katika muda wa saa 24 imekuwa ya kutia wasiwasi na saa 48 zijazo zitakuwa muhimu sana,” alisema na kuongeza: “Tuko mbali sana kusema yuko karibu kupona.”