Kimataifa

Trump ampiga kalamu mshauri wa masuala ya usalama

September 10th, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na AFP

RAIS wa Amerika Donald Trump amemfuta kazi mshauri wake kuhusu masuala ya Usalama wa Kitaifa John Bolton.

Rais Trump kupitia akaunti yake ya Twitter alisema ni yeye alimshauri Bolton ajiuzulu. Alisema Bolton alizingatia ushauri wake na kujiuzulu mnamo Jumanne asubuhi.

“Namshukuru John zaidi kwa huduma yake. Nitataja Mshauri wangu mpya wa Masuala ya Usalama wiki ijayo,” Trump akasema.

Akaongeza: “Nilimweleza John Bolton kwamba huduma zake hazihitajiki tana katika Ikulu ya Whit House. Nilipiga vikali baadhi ya mawaidha yake, jinsi nilipopinga ushauri kutoka kwa wengine katika serikali yangu.”

Lakini akijibu, Bolton alipinga kauli ya Trump akisema ni yeye aliyehiari kujiuzulu.

“Niliamua kujiuzulu Jumatatu usiku na Rais Trump akasema: ‘Tuzungumzie suala hilo kesho (Jumanne),” Bolton akaandikia katika akaunti yake ya twitter.

Hatua ya Trump kuamuru Bolton kujiuzulu inajiri huku mengi yakisemwa kuhusu msimamo wake kuhusu hatua ya Iran kutangaza kuwa ingeanza kuzalisha kawi ya nuklia.

Bolton alikuwa ametuma ujumbe, kupitia twitter, alishutumu Iran katika kile alichotaja kuwa “rundo la uwongo” kuhusu suala la mzozo nchini Syria, suala ambalo Trump alitofautiana nalo.

“Wakati huu ambapo zimesalia wiki mbili kabla ya kufanyika kwa Mkutano wa Mkuu wa Umoja wa Kimataifa (UNGA), fahamu kuwa Iran inafanya kila iwezalo kuhadaa,” Bolton akaandika

“Huku tukikumbuka wiki hii mashambulio la kigaidi nchini Amerika mnamo Septemba 9, 2011, ni muhimu kukumbuka hatua ambayo tumepiga kukamilia na makundi ya kigaidi na pia kazi ambayo imesalia. Tunapinga serikali zinazofadhili ugaidi na mashauri,” Bolton akaongeza.