HabariKimataifa

Trump amtimua Godec, ateua Kyle McCarter kutwaa nafasi yake

March 29th, 2018 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

RAIS Donald J. Trump Alhamisi amemfuta kazi Balozi wa Amerika nchini Kenya Robert Godec na nafasi hiyo akampa Seneta wa Illinois, Kyle McCarter.

Taarifa kutoka White House alisema Bw McCarter ana ufahamu kuhusu Kenya baada ya kuhudumu kama mmishonari na Mkurugenzi wa kampuni ya Each One Feed One International,iliyokuwa na afisi yake eneo la Mukothima,Kaunti ya Tharaka-Nithi.

“Seneta McCarter amefanya kazi na shule za kibinafsi za K-8 ambapo alisaidia watoto masikini na mayatima. Alitoa huduma za matibabu kwa zaidi ya watu 15,000 kila mwaka alipokuwa mkurugenzi wa Each One Feed One International,” ilinukuu taarifa ya Ikulu.

Katika mtandao wake wa Twitter, McCarter alimshukuru Rais Trump kwa uteuzi huo na kuelezea furaha yake ya kutumwa kuhudumu Kenya.

“Ni heshima kubwa kwa kutumwa na Rais Trump na taifa la Amerika kwenda kurudi kuhuduma taifa ambalo nimeishi na kufanya kazi,”alisema Bw McCarter.

Seneta huyo alisema anakusudia kukuza uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ili kuacha wosia unaompendeza Mungu na raia wa mataifa yote.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Amerika, McCarter na mkewe wanaongea Kiswahili sanifu baada ya kuishi Kenya kwa muda.

Uteuzi wa seneta huyo unatarajiwa kuidhinishwa na kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Kigeni nchini Amerika.

“Nina upendo mkubwa kwa Kenya,” McCarte aliambia gazeti moja nchini Amerika.

Baada ya kuidhinishwa na Seneti, McCarter atachukua mahali pa Bw Godec ambaye muhula wake nchini Kenya ulikumbwa na shutuma kutoka kwa muungano wa upinzani NASA uliodai kuwa anaegemea upande wa serikali.

Godec aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama mnamo 2012 kuwa balozi wa Kenya na kabla ya hapo alihudumu kama balozi wa Amerika nchini Tunisia kutoka 2006 hadi 2009.

Katika ujumbe wake wa kwaheri, Godec alisema anajivunia ushirikiano aliokuza mataifa hayo mawili katika nyanja za kilimo, afya, biashara, uwekezaji, usalama pamoja na uongozi.

“Kenya ina mahali pazuri katika moyo wangu. Ningependa kusema asanteni sana kwa serikali ya Kenya, raia wa Kenya na wenzangu katika ubalozi kwa ushirikiano mzuri wa zaidi ya miaka mitano niliyohudumu hapa,”alisema Bw Godec katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.