Kimataifa

Trump anapanga kumteua binti yake kuwa balozi UN

October 11th, 2018 2 min read

NA MASHIRIKA

WASHINGTON DC, AMERIKA

KIONGOZI wa Amerika Rais Donald, Trump amedokeza azma yake ya kumteua binti yake, Ivanka, kuwa balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua nafasi ya Nikki Haley aliyejiuzulu ghafla, Jumanne.

Rais Trump alisema alisema japo angependa kumteua binti yake kuwa balozi anahofia kuwa raia wa Amerika watamshutumu kwa mapendeleo.

“Ivanka anaweza kutumikia Amerika vyema ikiwa atateuliwa kuwa balozi katika UN. Si mapendeleo hata kidogo kwani Ivanka amehitimu. Hata Waamerika wanajua kwamba Ivanka ni mchapa kazi lakini bado watanishambulia kwa kuendeleza upendeleo,” akasema Trump alipokuwa akihutubu katika Ikulu ya White House.

Trump alisema hayo saa chache baada ya kutangaza kuwa amepokea barua ya kujiuzulu kwa Haley ambaye atang’atuka afisini kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

“Tunaendelea kutafuta mtu atakayejaza nafasi hiyo. Tunaendelea kutathmini watu mbalimbali akiwemo Ivanka,” Trump akaambia wanahabari.

Ikiwa Trump atamteua binti yake kuwa balozi wa Amerika katika UN, haitakuwa mara ya kwanza kwake kuchanganya biashara zake za kibinafsi na jamaa zake katika uendeshaji wa serikali yake tangu alipochaguliwa mnamo 2016.

Ivanka na mumewe Jared Kushner wanafanya kazi katika Ikulu ya White House kama washauri wa Trump japo hawapokei mshahara.

Kushner, ambaye ni Myahudi ndiye ametwika jukumu la kuandaa mipango ya kurejesha amani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Haley alikutana na Trump kabla ya kutangaza kujiuzulu. Trump alimmiminia sifa tele huku akisema kuwa alitumikia vyema Amerika katika UN.

“Haley alinieleza miezi sita iliyopita kuwa anataka kupumzika,” akasema Trump.

Mrithi wa Haley anatarajiwa kutajwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Kufikia sasa Haley hajaweka wazi sababu yake ya kujiuzulu.

Vyombo ya habari nchini Amerika vilisema kuwa kujiuzulu kwa Haley kulimshangaza hata waziri wa Mashauri ya Kigeni wan chi hiyo Mike Pompeo.

Ripoti za vyombo vya habari pia zilidai kuwa Haley alijiuzulu ili kujiandaa kumenyana na Rais Trump katika kinyang’anyiro cha urais 2020.

Lakini Haley alikanusha madai hayo kwa kusema: “La hasha, sitawania urais 2020.”

Trump alisisitiza kuwa balozi huyo alijiuzulu kwa hiari na wala hakushinikizwa.