Kimataifa

Trump aonya Iran dhidi ya kuua waandamanaji

January 13th, 2020 1 min read

NA AFP

RAIS wa Donald Trump wa Marekani ameionya Iran dhidi ya kuwaua waandamanaji wanaolaani kuangushwa kimakosa kwa ndege ya Ukraine wiki iliyopita.

Baadhi ya raia wa Iran wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali yao ambayo ilikiri kuangusha ndege ya Ukraine kimakosa.

Ndege hiyo iliangushwa kwa makombora yaliyolenga kulipiza kisasi mauaji ya kamanda wao wa kijeshi Qasem Soleimani majuma mawili yaliyopita.

“Naionya vikali Iran dhidi ya kuwaua raia wake wanaoandamana kupinga kuangushwa kwa ndege ya Ukraine. Marekani inatazama na kufuatilia kwa makini hatua zozote mnazopanga kuchukua,” akaandika Trump kwenye Twitter.

Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya abiria 176, wengi wao raia wa Iran na tayari serikali imeomba radhi kuhusu kisa hicho.

Kupitia mahojiano na vyombo vya habari, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper alisema Rais Trump bado alikuwa akisubiri kuandaa mazungumzo na viongozi wa Iran licha ya uhasama kati ya mataifa hayo kufuatia mauaji ya Soleimani jijini Baghdad nchini Iraq mnamo Januari 3.

“Tuko tayari kuketi chini nao na kujadili masuala yanayozua taharuki kati yetu. Hata hivyo, hatutafanya hivyo wakitupa masharti makali kabla ya mazungumzo,” akasema Esper.

Aliongeza kuwa Rais Trump hajabainisha wazi hatua atakayochukua iwapo serikali ya Iran itawakabili waandamanaji hao.

Balozi wa Marekani nchini Iran alikamatwa mnamo Jumamosi na kuachiliwa baada ya kuhudhuria ibada ya mazishi ya waliouawa kwenye ndege ya Ukraine, hafla iliyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Amir Kabir.

Kwa mujibu wa Esper, maandamano nchini Iran hayajachochewa na kisa hicho cha ndege pekee bali ufisadi uliogubika serikali ya Rais Hassan Rouhani wa Iran.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Robert O’Brien naye alikejeli Iran akisema kwamba serikali hiyo haitakuwa na budi ila kukubali mazungumzo kutokana na shinikizo za waandamanaji.

“Iran inaendelea kulemewa na haitakuwa na budi ila kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Raia wa nchi hiyo wamechoshwa na uongozi mbaya,” akasema O’Brien.