Kimataifa

Trump apata afueni korti ikimpa kinga dhidi ya kushtakiwa kwa uvamizi wa Bunge

Na MASHIRIKA July 2nd, 2024 2 min read

WASHINGTON, AMERIKA

MAHAKAMA ya Juu ya Amerika Jumatatu ilitoa maamuzi kuwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump ana kinga na kwamba hawezi kufunguliwa mashtaka kwa matendo yoyote rasmi aliyofanya ya kujaribu kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema kuwa mwanasiasa huyo anayekabiliwa na kesi kadhaa hana kinga kwa matendo yasiyo rasmi aliyoyachukuwa akiwa uongozini.

Mahakama hiyo imeziachia mahakama za chini kufanya maamuzi ni kesi zipi ambazo Trump anaweza kufunguliwa mashtaka.

Uamuzi huo wa majaji 6 umemhakikishia Trump kuwa hatashtakiwa katika kesi kabla ya uchaguzi wa Novemba 5 ambapo yeye ni mgombea mteule wa chama cha Republican huku akitarajiwa kukabiliana na Rais Joe Biden, aliyemshinda katika uchaguzi wa 2020.

“Tunahitimisha kuwa chini ya muundo wetu wa kikatiba rais wa zamani ana kinga ya kutoshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa vitendo rasmi alivyofanya akiwa uongozini,” jaji John Roberts aliandika.

Trump alipongeza uamuzi huo akisema huo ni ushindi mkubwa kwa demokrasia ya nchi hiyo.

Trump amekuwa akinusha kufanya kosa lolote linalohusishwa na matokeo ya uchaguzi wa 2020 lakini kwa muda mrefu amekuwa akidai kulikuwa mchakato wa kupiga kura na kuhesabiwa kwa kura ulikumbwa na matatizo kadhaa jambo awapo Trump ataibuka mshindi katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, basi huenda akamtumia mwanasheria wake mkuu na mwendesha mashtaka mkuu ili ‘kujitakasa’ na iwapo atashindwa, basi mwanasiasa huyo ataanza kukabiliwa na kesi hiyo ya 2020.

Mahakama Kuu ilikuwa ya kwanza kufanya maamuzi iwapo rais huyo wa zamani huenda akashtakiwa kwa kesi ya uhalifu kwa vitendo alivyofanya akiwa madarakani, au kama ana kinga ya kumzuia kushtakiwa.

Msingi wa sheria za Amerika unaelezea wazi kwamba hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria, kuwa kila mtu ana uhuru sawa lakini pia kila mtu anaweza kushtakiwa kwa kuvunja sheria.

Trump alidai kuwa ana kinga kwa maamuzi aliyofanya wakati huo, akisema kwamba si haki ashtakiwe kwa kujaribu kubadilisha matokeo ya uchaguzi, kwani alikuwa akichukua hatua kama rais akijaribu kuimarisha uadilifu katika matokeo, akisisitiza kwamba alishindwa kwa sababu ya wizi na matatizo mengine katika uchaguzi.

Mwanasheria maalum wa Wizara ya Sheria, Jack Smith alimshutumu Trump katika makosa manne yaliyowasilishwa huko Washington karibu mwaka mmoja uliopita kwa njama ya kutaka kubadili mtokeo ya uchaguzi wa 2020 ili abaki madarakani.

Haya yanajiri huku Trump na mhasimu wake wa kisiasa Biden wakiendeleza kampeni katika maeneo mbalimbali wakijaribu kuuza sera zao kwa wananchi.