Kimataifa

Trump 'ashindwa kupumua’ baada ya kurudi White House

October 7th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON DC, Amerika

RAIS wa Amerika Donald Trump jana Jumanne alionekana “aking’ang’ana kupumua” huku akiwa amesimama kwa ukakamavu nje ya Ikulu ya White House bila kuvalia maski.

Rais huyo alichanachana magwanda yaliyokuwa yamemfunika aliporejea katika makao yake rasmi jijini Washington DC siku tatu tu baada ya kulazwa hospitalini kuhusiana na virusi vya corona.

Alieleza vyombo vya habari nchini humo kuwa “alihisi vyema kabisa” na hakuwa amesimama karibu na mtu yeyote ambaye hakuwa amevalia maski.

Hata hivyo, alifanya hivyo siku moja tu baada ya kudai kuwa sasa “amepata” virusi vya corona ambavyo vimewaua Waamerika 210,000.

Huku akiwa amesimama kwenye vidato hivyo maarufu, watu waliashiria kuwa rais huyo alikuwa akipumua kwa nguvu na “kusonya kwa maumivu,” pengine kudhihirisha kwamba bado alikuwa akiugua kutokana na athari za virusi hivyo.

Hali inayoitwa ‘Covid ndefu’ imewaacha wagonjwa wengi wa virusi vya corona wakiwa na matatizo ya kuishiwa na hewa, uchovu mbaya na mduwazo wa ubongo miezi kadhaa baada ya kuugua virusi hivyo.

Dkt Zoe Norris alisema Trump hakuonekana mzima katika picha na video zilizorekodiwa kutoka White House.

“Ni wazi kuwa anatatizika kupumua. Huyo si mtu aliyepata nafuu,” alisema.

Trump anasemekana kuhofia kuonekana ‘mnyonge’ katika wiki tatu muhimu kabla ya uchaguzi mnamo Novemba 3, 2020, huku akiandika kupitia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, akiwaeleza Waamerika “msiogope.”

Hasimu wake wa chama cha Democrat Joe Biden alikashifu mwelekeo wa Rais huyo wa ‘kujishajiisha’ unaoepuka kuvalia maski, akisema ‘alichangia’ kuambukizwa kwake.

“Mtu yeyote anayepata virusi kwa kusema kwamba ‘maski si muhimu, kujitenga kutangamana kijamii si muhimu,’ nafikiri anachangia kinachomtendekea,”

“Kujishajiisha huku ni nini, ‘sitavalia maski?’ Nini cha mno hapa?  Maski inakuumiza? Kuwa mzalendo jameni! Jilinde, lakini pia uwalinde majirani zako,” alisema Biden.

Licha ya rais huyo kurejea kwa ukaidi, bado haijulikani ni lini mara ya mwisho vipimo vyake vilipoonyesha hana virusi vya corona, huku watu 14 katika ikulu ya White House – akiwemo Mama Taifa Melania Trump – wakipatikana na virusi hivyo.

Trump aliondoka hospitali ya Walter Reed eneo la Bethesda, Maryland, mnamo Jumatatu, akipitia katika kijisehemu cha jeshi katika malango ya mbele ya hospitali hiyo, kabla ya kuelekea katika gari lisilopitisha risasi.

Rais huyo hakujibu swali kuhusu idadi ya wafanyakazi wa White House walioambukizwa au ikiwa yeye ni ‘msambazaji sugu’ aliyekuwa amewaambukiza virusi vya corona watu wengine wengi alipokuwa akitoka kituo hicho cha kifahari.