Trump ataka teknolojia ya 6G hata kabla ya kuonja 5G

Trump ataka teknolojia ya 6G hata kabla ya kuonja 5G

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WASHINGTON, MAREKANI

RAIS wa Amerika Donald Trump anawataka wakali wa teknolojia sasa kutengeneza mfumo wa intaneti wa 6G, ambao utakuwa na nguvu na kasi zaidi ya kupenyeza mitandaoni, kuliko viwango vya sasa.

Rais Trump amezitaka kampuni za Marekani kuboresha ubunifu, kabla taifa linguine lije na intaneti hiyo, akisema “hakuna sababu yoyote kwetu kuachwa nyuma.”

Alisema anataka kuona intaneti ya 6G ikifanya kazi huko Marekani “haraka iwezekanavyo.”

Bw Trump alisema hivi kupitia jumbe za Twitter, wakati ikidhaniwa kuwa Rais huyo amehofishwa na teknolojia ya kampuni za China kama Huawei, ambazo zimekuwa kipaumbele katika utumiaji na uuzaji wa intaneti ya 5G.

Mnamo 2018, kuliibuka duru kuwa US ilikuwa ikipanga kujitengenezea intaneti yake ya 5G, kwa hofu kuwa “China imemiliki utengenezaji na usimamizi wa mitambo ya mawasiliano.”

Trump kwenye jumbe za Twitter alisema kuwa anataka Amerika kushinda vita vya intaneti. “Nataka US ishinde mashindano si kwa kuzuia teknolojia zilizoendelea kwa sasa.”

Matamshi yake, hata hivyo, ni kinyume na ripoti kuwa Amerika inapanga kuzuia kampuni za China kuweka mitambo yake ya kusaidia utekelezaji wa teknolojia ya 5G kufanya kazi huko.

Hata hivyo, japo Rais Trump anapendekeza kampuni za nchi yake zitengeneze intaneti hiyo ya 6G, bado hakuna yeyote aliyewazia wala kueleza namna hilo linaweza kufanywa.

Idara ya mawasiliano ya kiteknolojia US imedinda kuzungumzia suala la Rais Trump kutaka intaneti ya 6G kutengenezwa, ikishikilia kuwa nchi hiyo iko mbioni kuhakikisha kuwa ile ya 5G inawekwa vyema.

You can share this post!

JUDITH OSIMBA: ‘De Gea’ wa Harambee Starlets...

Mashabiki wa raga wamwomboleza Richard Sidindi Otieno

adminleo