Habari

Trump atishia kuelekea mahakamani timu ya Biden ikikosoa matamshi yake

November 4th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

RAIS wa Amerika Donald Trump anayetetea wadhifa wake kwa tiketi ya chama cha Republican amesema atapinga katika mahakama ya juu zaidi matokeo ya uchaguzi, hata kabla shughuli za kuhesabu kura kukamilika.

Taifa hilo lilishiriki uchaguzi wa urais jana Jumanne ambapo Rais Trump anatoana kijasho na aliyekuwa Makamu wa Rais, Joe Biden wa Democratic.

Hata ingawa matokeo rasmi hayajatolewa wala kutangazwa, matokeo ya ziada shughuli za kuhesabu kura zikiendelea yanaonyesha Biden anaongoza. Amerika ina majimbo 50.

Mapema Jumatano, Donald Trump amedai kuwa tayari ameshinda uchaguzi huo, katika hotuba aliyoitoa White House hata kabla ya mamilioni ya kura kuhesabiwa.

Rais huyo amesema ataelekea katika mahakama ya juu zaidi Amerika kupinga matokeo, akitaka shughuli za kuhesabu kura zisitishwe kwa kile amedai shughuli hiyo “imekumbwa na udanganyifu”.

“Kuna udanganyifu mkubwa hapa nchini. Tutaelekea katika mahakama ya juu zaidi shughuli za kuhesabu kura zisimamishwe. Inahuzunisha,” Bw Trump akasema.

Hotuba yake imesababisha mfadhaiko wa akili kwa wafuasi wake, huku hofu ya mchipuko wa ghasia Amerika ikinukia.

Huku kukiwa na kura nyingi ambazo hazijahesabiwa, Trump amedai kuwa ameshinda.

“Ukweli ni kwamba tumeshinda, uchaguzi umekumbwa na udanganyifu. Hii ni aibu kwa nchi yetu,” akaelezea, bila kutoa ushahidi wa madai ya wizi wa kura.

Kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, mapema Jumatano alichapisha: “Tuko mbele, lakini wanajaribu kuiba uchaguzi (akimaanisha kura). Hatutawaruhusu wafanye hivyo. Kura haziwezi kupigwa baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa”.

Kwa upande wa mgombea urais wa Democratic Joe Biden, timu yake ya kampeni imemchamba Trump aliyetishia kuelekea mahakamani, ikisema ina mawakili ambao watapambana vilivyo kisheria kuhakikisha kila kura inahesabiwa.

“Hotuba ya Rais usiku huu wa kuamkia Jumatano kwamba ananuia kuhakikisha mchakato wa kujumuisha kura unasitishwa ni ya kukera na hapajawahi kutokea kitu kama hiki, lakini pia haina msingi,” amesema meneja wa kampeni ya Biden Jen O’Malley Dillon kupitia taarifa aliyoitoa.

Akaongeza: “Hakuna popote katika historia ya Amerika ambapo Rais alizima sauti ya Waamerika katika shughuli ya uchaguzi wa kitaifa.”

Dillon aidha amesisitiza kwamba Trump hana mamlaka ya kujitangaza mshindi ili kuonekana kuelekeza ushawishi wake katika ujumuishaji kura zilizopigwa.