Habari Mseto

Trump azidi kukaa ngumu

November 9th, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA Na AFP

Rais wa Amerika, Donald J Trump amekataa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa urais hata baada ya mpinzani wake mkuu Joe Biden kutangazwa mshindi.

Msimamo wa rais huyo umemfanya atengwe na baadhi ya washauri na washirika wake ambao wamempongeza Biden.Trump alisisitiza kuwa, alishinda uchaguzi huo kwa kura nyingi ingawa maafisa wakuu wa chama chake cha Republican walijitenga na msimamo wake na kumpongeza Biden.

Duru zilisema kwamba, baadhi ya washauri wake wa karibu pia walijitenga na kauli zake za kukosoa uchaguzi huo ambao alibwagwa na Biden wa chama cha Democratic hata katika ngome zake.

Biden alipata kura 290 za wajumbe dhidi ya 214 za Trump. Katika uchaguzi wa urais Amerika anayepata kura 270 wa kwanza huwa anatangazwa mshindi.

“Nilishinda uchaguzi huu kwa kura 71 milioni ambazo hakuna rais mwingine wa Amerika anayehudumu aliwahi kushinda kwenye uchaguzi,” Trump aliandika kwenye Twitter wakati wafuasi wa Biden walikuwa wakisherehekea ushindi wa makamu huyo wa rais wa zamani.

Aliibua madai mapya ambayo hakuweza kuthibitisha kwamba, waangalizi wa uchaguzi wa chama chake hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya kuhesabia kura.

“Mambo mabaya yalitendeka ambayo waangalizi wetu hawakuruhusiwa kuona. Haya hayajawahi kutendeka. Mamilioni ya karatasi za kura yalitumwa kwa watu ambao hawakuitisha,” alisema akirejelea upigaji kura wa mapema kwa njia ya posta ambao amekuwa akidai ulitumiwa kuiba kura.

Huku akiteta na kukaa ngumu, risala za kumpongeza Biden ziliendelea kumiminika kutoka kote ulimwenguni. Miongoni mwa waliompongeza Biden ni maseneta wa Republican wenye ushawishi wakiongozwa na Mitt Romney.

Aliyekuwa rais George Bush pia wa chama cha Republican alimpongeza Biden.Rais huyo mbishi hakuonekana kulegeza msimamo hata raia wa nchi hiyo walipomiminika barabarani kote katika miji kusherehekea ushindi wa Biden.

“Ukweli wa kimsingi kabisa ni kuwa, uchaguzi huu haujakamilika. Joe Biden hajaidhinishwa kuwa mshindi na jimbo lolote hata yale ambayo hakuna mzozo na yale ambayo kura zitahesabiwa tena na kuna uwezekano wa mshindi kuamuliwa na korti,” alisema.

Inasemekana Trump anajiandaa kuelekea kortini Jumatatu kupinga ushindi wa Biden juhudi ambazo zinaongozwa na mwana mkwe wake Jared Kushner, wanawe Donald Trump Jr na Eric Trump na aliyekuwa meya wa New York Rudy Giuliani.

Hata hivyo wadadisi wanasema huenda juhudi hizo zikagonga mwamba kwa kukosa mchango wa mawakili wenye uzoefu mkubwa ambao inasemekana wamemhepa.

Inasemekana licha ya kukosa kulegeza msimamo, Trump anategemea washauri wa kifamilia. Baadhi ya vyombo vya habari jana viliripoti kuwa Kushner alikuwa akiwaza kumshauri Trump kubadilisha msimamo na kukubali kushindwa.

James Baker aliyeongoza kesi ya uchaguzi ya mgombeaji wa kiti cha Republican George Bush dhidi ya Al Gore wa chama cha Democratic miaka 20 iliyopita alipuuza kauli za Trump akisema hazina mashiko.

Duru zilisema alikataa wito wa Kushner kuwakilisha Trump katika kesi kortini.Washauri wenye uzoefu wa Trump wamesema hatafua dafu katika juhudi zake kortini.