Habari

Trump azimwa

November 7th, 2020 2 min read

Na AFP

WASHINGTON D.C., Amerika

VITUO kadhaa vya runinga nchini Amerika vilikatiza kupeperusha moja kwa moja hotuba ya Rais Donald Trump, baada ya kugundua kwamba alikuwa akieneza habari za uongo.

Trump alitoa madai yasiyoweza kuthibitishwa katika hotuba yake iliyochukua dakika 17 akisisitiza kuwa chama cha Democratic kilikuwa kikitumia kura haramu kumpokonya ushindi.

Alitoa hotuba hiyo wakati ambao kura zilizokuwa zikiendelea kuhesabiwa katika majimbo yenye ushindani mkali, zilionyesha kwamba Joe Biden wa chama cha Democratic alikuwa akielekea kushinda.

“Basi, kwa mara nyingine, tumejipata katika hali isiyo ya kawaida sio tu kukatiza hotuba ya rais wa Amerika lakini pia kumrekebisha rais wa Amerika,” alisema mtangazaji wa runinga ya MSNBC Brian Williams, kituo hicho kilipokatiza haraka kupeperusha hotuba hiyo.

Vituo vya runinga vya NBC na ABC News pia viliacha kupeperusha moja kwa moja hotuba ya Trump.

“Ni usiku wa huzuni ulioje kwa Amerika kusikia rais wao akieneza uongo akilaumu watu kwa kujaribu kudanganya katika uchaguzi,” alisema mtangazaji wa runinga ya CNN Jake Tapper.

Alitaja matamshi ya Trump kuhusu wizi wa kura kama uongo baada ya uongo ambao hauwezi kuthibitishwa kabisa.

Rais huyo aliropokwa madai yasiyoweza kuthibitishwa kwamba amepokonywa ushindi katika uchaguzi wa urais wa Amerika wakati ambao kura zilikuwa zikiendelea kuhesabiwa katika majimbo yenye ushindani Ijumaa na kuonyesha kwamba Biden alikuwa akiongoza.

“Wanajaribu kuiba kura,” alisema Trump ambaye anaendelea kutengwa akihutubu kutoka Ikulu ya White House Alhamisi, siku mbili baada ya kura kupigwa.

Bila kutoa ushahidi wowote na kukataa maswali kutoka kwa wanahabari, Trump alitumia dakika 17 kuropokwa madai ya kulaumu mfumo wa demokrasia ambayo hayajawahi kutamkwa na rais mwingine wa Amerika.

Kulingana na Trump, chama cha Democratic kilikuwa kikitumia kura haramu ili kupokonya ushindi chama chake cha Republican.

“Ukihesabu kura halali, ninashinda kwa urahisi sana,” alidai. “ Wanajaribu kudanganya katika uchaguzi, na hatutakubali hilo kufanyika,” alipayuka.

Madai hayo, ambayo yalichapishwa kwenye Twitter Ijumaa asubuhi yalijiri wakati wakuu wa kampeni yake walikuwa wakiendelea kupinga uhalali wa kura nyingi zilizopingwa kwa njia ya posta kuliko tarehe ya uchaguzi.

Watu wengi waliamua kupiga kura mapema mwaka huu wakihofia kuambukizwa corona kwenye misongamano ya watu katika vituo vya kupigia kura. Ugonjwa huo umeua watu 235,000 nchini Amerika.

Wafuasi wengi wa chama cha Democratic ndio waliopiga kura kwa wingi kutumia posta. Katika jimbo la Pennsylvania, wafuasi wa Trump walijaribu kusimamisha kuhesabiwa kwa kura.

Viongozi wa kampeni ya Trump walisisitiza kuwa ni lazima ashinde wakitaja idadi kubwa ya kura katika ngome za chama cha Republican ambazo hazikuwa zimehesabiwa na kudai kulikuwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote.

Wandani wa Trump walipinga matokeo kortini katika majimbo hayo na kupiga kambi nje ya ofisi za uchaguzi katika miji kadhaa.

Nje ya ofisi moja katika mji mkuu wa jimbo la Arizona, Phoenix, mkereketwa kwa chama cha Republican Alex Jones aliongoza umati wa watu waliokuwa na silaha akiropokwa kupitia spika kubwa akilenga wanaochukulia kuwa maadui wa Trump “Wataharibiwa kwa sababu Amerika inainuka,” alisema.

Katika jiji la Las Vegas, wafuasi wa Trump walitaka waruhusiwe kushuhudia kura zikihesabiwa.