Kimataifa

Trump kupatanisha Misri, Ethiopia kuhusu mto Nile

November 7th, 2019 2 min read

NA AFP

MAWAZIRI kutoka Misri, Ethiopia na Sudan jana walikutana jijini Washington DC kujaribu kutatua mzozo kuhusu ujenzi wa bwawa ndani ya Mto Nile.

Misri na Sudan zinapinga hatua ya Ethiopia kujenga bwawa la Grand Renaissance ndani ya Mto Nile. Iwapo ujenzi huo utakamilika, bwawa la Grand Renaissance ndilo litakuwa kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha kawi ya umeme barani Afrika. Bwawa hilo litazalisha 6,000 megawati za umeme.

Misri ambayo hupata asilimia 80 ya maji yake kutoka Mto Nile inahofia kwamba, bwawa hilo la Ethiopia litasababisha uhaba wa maji.

Amerika imejitolea kupatanisha mataifa hayo mawili baada ya mikutano ya hapo awali kuambulia patupu.

Ethiopia inataka kujenga bwawa hilo lililogharimu Sh400 bilioni ndani ya kipindi cha miaka sita lakini Misri inataka ujenzi huo ucheleweshwe kwa angalau miaka 10 ili kujadili namna ya kuhakikisha kuwa mataifa mengine yanayonufaika na maji ya mto huo hayaathriwi.

Mradi huo ukikamilika, Ethiopia itauza kawi ya umeme katika mataifa jirani kama vile Kenya, Tanzania, Somalia, Djibouti nakadhalika.

Rais wa Amerika Donald Trump mapema wiki hii aliingilia mzozo huo akisema kuwa anaunga mkono mazungumzo kati ya Misri, Ethiopia na Sudan kuhusu ujenzi wa bwawa.

Kabla ya mkutano wa jana, Rais Trump alimpigia simu kiongozi wa Misri Rais Abdel Fattah el-Sisi ambapo walijadili kwa kina mzozo kuhusu ujenzi wa bwawa katika Mto Nile.

“Rais Trump anaunga mkono mazungumzo kuhusu ujenzi wa Bwawa la Renaissance ili kutafuta suluhisho,” ikasema taarifa ya Ikulu ya White House.

Rais El-Sisi alimshukuru Rais Trump kupitia mitandao ya kijamii kwa kujitolea kupatanisha mataifa hayo matatu.

Mawaziri wa Misri, Ethiopia na Sudan walikutana jijini Washington DC kufuatia mwaliko wa Rais Trump.

Ethiopia inasisitiza kuwa mradi huo utaisaidia pakubwa kustawi kiuchumi.

Amerika iliingilia kati baada ya Misri kusisitiza kuwa pande husika zipatanishwe na mpatanishi kutoka nje.

Awali, serikali ya Amerika ilikuwa imepuuzilia mbali wito wa Misri kutaka kupatanishwa na mataifa ya kigeni.

Mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliambia Bunge kuwa yuko tayari kutuma majeshi yake kupigana ili kuhakikisha kwamba mradi huo unaendelea.

Abiy, ambaye alituzwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu, hata hivyo, alisema kuwa watafanya mazungumzo na Misri na Sudan ili kutafutia ufumbuzi mzozo huo.

Kauli hiyo ilighadhabisha Misri ambayo iliyataja kuwa ya ‘kiholela’.