Trump kwisha!

Trump kwisha!

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

JUHUDI za mwisho za Rais Donald Trump wa Amerika kukatalia madarakani ziligonga mwamba Alhamisi, licha yake kutumia ghasia zilizosababisha vifo vya watu wanne jijini Washington.

Tukio hilo linamweka kiongozi huyo mzushi na mwenye madaha kwenye hatari ya kufunguliwa mashtaka ya jaribio la kuhujumu katiba ya nchi hiyo, kuchochea fujo pamoja na makosa mengine.

Ghasia hizo za wafuasi wake pia zilizua mjadala kuwa makamu wake Mike Pence atumie sheria inayomruhusu kumwondoa rais madarakani iwapo atakuwa tishio kwa usalama ama kushindwa kuongoza kisheria.

Ripota wa CNN alieleza kuwa kulikuwa na wasiwasi Trump hakuwa sawa kiakili, na hivyo huenda akatenda jambo lenye madhara kwa Amerika na dunia.

Ghasia za Jumatano zilikuwa aibu kubwa kwa Amerika ambayo hujidai kwa ustawi wa demokrasia.

Maafisa kadhaa wa serikali ya Trump walijiuzulu kufuatia ghasia hizo.

Kulingana na ‘Al Jazeera’, kati ya waliojiuzulu ni Naibu Mshauri wa Usalama, Matt Pottinger, Mkuu wa Watumishi wa Mkewe Rais, Melania, Stephanie Grisham, Katibu wa Kijamii katika White House Anna Cristina Niceta na Naibu Msemaji wa White House Sarah Matthews.

Waandamanaji waaminifu kwa Trump walitii mwito wake wa kuvamia makao ya bunge wakati makamu wake, Pence alipokuwa akiongoza kikao cha pamoja cha Seneti na Bunge la Waakilishi, cha kuidhinisha ushindi wa Biden kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 3, mwaka jana.

Uvamizi huo ulilazimisha kuondolewa kwa maseneta na wabunge kwenye makao hayo, lakini wakarejea baada ya masaa kadhaa utulivu uliporejelewa na kuendelea na shughuli ambapo Biden aliidhinishwa kuchaguliwa kwa njia halali.

CNN iliripoti kuwa Trump alikuwa amekataa kuidhinisha kikosi cha National Guard kutumwa kukabili waandamanaji baada ya polisi kulemewa.

Baadaye rais huyo aliwashukuru wahuni hao ambao waliharibu mali na kutatiza shughuli za bunge.

Jumatano mitandao ya ‘Twitter’ na ‘Facebook’ ilifunga kwa muda akaunti za Trump kwa “kueneza jumbe za chuki na kushabikia ghasia.”

Kwa kawaida kikao cha pamoja cha kuidhinisha mshindi wa urais huwa ni cha amani na ustaarabu, lakini jana kiliahirishwa kwa masaa kadhaa baada ya waandamanaji kuvunja na kuingia ndani.

‘New York Times’ ilieleza kuwa wafuasi wa Trump walipora ofisi ya Spika wa Bunge la Waakilishi Nancy Pelosi kwa kuvunja vioo na kuiba vitu kadhaa kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mijadala wa bunge wakiwa wamebeba bendera zenye picha ya Trump.

Tukio hilo lilishutumiwa na wabunge na maseneta wa vyama vya Democratic na Republican kwa pamoja.

“Kwa wale ambao wamezua fujo katika bunge leo, hamkushinda. Ghasia kamwe haziwezi kushinda. Uhuru ndio ushindi,” akasema Pence.

Hayo yalitokea siku ambayo chama cha Democratic kilishinda viti viwili vya useneta katika jimbo la Georgia na hivyo kuchuka usukani wa Seneti.

Ghasia hizo zilichochewa na Trump ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya uongo akidai alipokonywa ushindi na kuhimiza wafuasi wake watumie kila mbinu kupinga.

Katika hatua moja Trump aliwataka wafuasi wake kuwakabili viongozi wa chama chake cha Republican ambao hawakubaliani naye.

Wakati wa uidhinishaji wa matokeo, maafisa wa Republican wa majimbo ya Arizona na Pennsylvania walipinga na kulazimisha mjadala lakini wakashindwa kwenye kura.

Baadaye Rais Trump alisalimu amri na kutangaza kuwa atakabidhi madaraka kwa Joe Biden hapo Januari 20 kwa njia ya amani.

Hii ni baada ya kiongozi huyo mtukutu na mbishi kushindwa katika juhudi zake za mwisho za kuvuruga ushindi wa Biden, alipochochea wafuasi wake kuvamia kikao cha pamoja cha Seneti na Bunge la Waakilishi kwa nia ya kusimamisha shughuli hiyo.

Lakini makamu wake, Mike Pence alisimama kidete na kutangaza kuwa ataheshimu katiba wala sio maslahi ya mtu binafsi.

You can share this post!

Ugavana wa Nairobi wazidi kukanganya

KENNEDY OSORE: Soka inavyokuza maadili katika jamii