Kimataifa

Trump sasa apuliza hapa aking'ata kule

November 25th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON, Amerika

RAIS wa Amerika, Donald Trump amekubali serikali yake imsaidie Rais Mteule Joe Biden kujiandaa kutwaa mamlaka ya uongozi wa nchi, licha ya kuwa angali anasisitiza kupinga matokeo ya uchaguzi.

Trump alikiri kushauri Idara ya Kusimamia Huduma za Jumla serikalini (GSA) kuondoa kizuizi kilichowekwa ghafla kuhusu kumsaidia Biden.

Alisema kwamba wakati umewadia kwa GSA “kufanya kinachohitajika kufanywa”.

Hata hivyo, katika mtandao wa kijamii wa Twitter, alisisitiza kwamba bado anakataa kukiri kushindwa akisema, “Kesi yetu inaendelea vyema, tutaendelea na vita vyetu vizuri na ninaamini tutafaulu!”

Kwa mwanachama huyo wa Republican kuafikiana na uamuzi wa GSA wa kushirikiana na kikosi kipya cha Biden, kunaashiria kwamba hata yeye anaona ishara dhahiri baada ya wiki tatu za kutoa madai bila ushahidi wowote kwamba aliibiwa uchaguzi wa Novemba 3.

Aidha, inamaanisha kuwa kikosi cha Biden sasa kitaweza kutumia hela, afisi na kukutana na maafisa wa serikali. Afisi ya Biden iliyokuwa imetangaza saa kadhaa awali maafisa wenye tajriba kuu watakaoteuliwa katika nyadhifa kuu za sera ya kigeni na usalama Amerika, ilisema GSA sasa itaruhusu “msaada unaohitajika kuwezesha mchakato wa ubadilishanaji mamlaka kwa njia shwari na ya amani,”

“Katika siku zijazo, maafisa wanaohusika na ubadilishanaji mamlaka wataanza kukutana na maafisa wa kiserikali kujadili jinsi ya kukabili janga la corona, kupata ripoti kamili kuhusu usalama wetu wa kitaifa na kuelewa kikamilifu juhudi za usimamizi wa Trump za kukwamua mashirika ya kiserikali,” alisema Mkurugenzi wa Biden kuhusu ubadilishanaji mamlaka Yohannes Abraham, kupitia taarifa.

Mabadiliko hayo yalijiri baada ya eneo la Michigan kuwa la hivi karibuni kuidhinisha matokeo yake huku wafuasi zaidi wa Trump wakijitokeza na kutaka mvutano huo kufika kikomo.

Awali, Biden alitangaza kikosi cha kushughulikia sera ya kigeni na usalama wa kitaifa iliyojaa viongozi wa zamani kutoka enzi ya Barack Obama, hali iliyoashiria mwisho wa misukosuko chini ya uongozi wa Trump na kurejelewa kwa diplomasia iliyozoeleka Amerika.