Habari Mseto

TSC kuajiri walimu wapya kujaza nafasi za wale watakaogoma Januari

December 21st, 2018 1 min read

Na Ouma Wanzala

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imetengaza kuanza kuajiiri walimu hata ingawaje walimu wanatarajiwa kugoma kuanzia Januari mwaka ujao.

Jana, tume hiyo ilisema kwamba imeanza kupokea maombi ya kazi ili kujaza nafasi 1, 197 za walimu ambao wameondoka kutokana na sababu mbalimbali katika muda wa miezi mitatu iliyopita.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bi Nancy Macharia, nafasi 893 zimo katika shule za msingi huku 304 zikiwa katika shule za upili.

Alisema kuwa watakaotuma maombi wanapaswa kuwa wasiozidi umri wa miaka 45, na lazima wawe na stakabadhi zote muhimu kulingana na kanuni za tume. Kando na hayo, lazima wawe wamesajiliwa rasmi nayo, kulingana na Kipengele 23 cha sheria zake.

“Wanaotuma maombi ya kuwa walimu wa shule ya msingi lazima wawe na vyeti vya kiwango cha ualimu cha P1. Watateuliwa kutoka orodha ya kaunti iliyotayarishwa kwenye shughuli ya kuwaajiri walimu mnamo Mei mwaka huu.”

 

Wale wanaotuma maombi ya kuwa walimu wa shule za upili lazima wawe wamefikisha elimu yao katika kiwango cha diploma.

Wale watakaozingatiwa ni waliohojiwa na wamekuwa wakingoja kutumwa katika shule watakakofunzia.

Wale wanaopanga kutuma maombi yao waliagizwa kufanya hivyo kufikia Januari 4. Watatuma maombi hayo kwa makatibu wa bodi simamizi za shule hizo na wakurugenzi wa kaunti wa ATSC.

Bi Macharia alisema kwamba walimu watakaofaulu watatumwa katika sehemu yoyote nchini.

Mnamo Jumatano, Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kilitangaza mgomo kuanzia Januari 2, kikipinga hatua ya tume hiyo kuwaajiri walimu zaidi ya 3,904.

Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Sossion alisema kuwa taratibu zifaazo hazikuzingatiwa.