Habari

TSC kufunza walimu kuhusu CBC, kiwango cha Gredi 4

December 31st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TIME ya Huduma kwa Walimu (TSC) itaendesha mafunzo ya walimu 106,320 kuhusu mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) kuanzia Januari 2 hadi Januari 5, 2020.

Kwenye taarifa iliyotoa Jumanne, tume hiyo imesema kuwa walimu hao watatoka shule za umma na za binafsi.

Aidha, watajumuisha walimu wakuu na wakufunzi kutoka shule za wanakosomea watoto wenye mahitaji maalum.

“Mafunzo hayo yatalenga mwalimu mmoja wa daraja la gredi 1, 2 na 3 kutoka kila shule ya umma na ya kibinafsi,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia.

Aliongeza kuwa walimu wawili wa daraja la gredi 4 kutoka kila moja ya shule ya umma na shule ya kibinfsi wapewa mafunzo.

Hii ni sehemu ya mayarisho ya kuanza kwa utekelezaji wa mtaala wa CBC katika kiwango cha gredi 4 katika mwaka wa 2020.

Mafunzio hayo ya walimu pia yatahudhuriwa na jumla ya walimu wakuu 22,830.

“Watakaofundishwa wanajumuisha walimu 68,490 pia walimu 18,000 na 7,000 kutoka shule za umma, za binafsi na zile za wanafunzi wenye mahitaji maalum mtawalia,” Dkt Macharia akaeleza katika taarifa hiyo.

Ameongeza kuwa tume hiyo tayari imewafundisha jumla ya wakufunzi wakuu (master trainers) 208 wa CBC katika ngazi ya kitaifa katikati mwa Desemba 2019.

Wakufunzi 124 kati yao waliwafundisha walimu wa shule za kawaida huuku 84 wakiwafunza walimu wa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Baadaye wakufunzi hawa wakuu waliwafundisha maafisa 1,063 wa kutekeleza mtaala na wakufunzi 1,320 wa mtaala wa CBC katika vituo 42 kote nchini mnamo Desemba 2019.

“Mafunzo haya yatawapa walimu maarifa na ujuzi hitajika kwa utekelezaji wa mtaala wa CBC katika kiwango cha Gredi 4, katika nyanja ya mafunzo na utahini, kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula wa kwanza mwaka mpya 2020,” akasema Macharia.

Yaliyomo kwenye ratiba ya mafunzo ya walimu kuhusu mtaala wa CBC yametayarishwa na Taasisi ya Utayarishaji Mtaala Nchini (KICD) huku masuala ambayo yatatumiwa kuwatahini wanafunzi yametayarishwa na Baraza la Kitaifa la Mitihani (Knec).

TSC hujkishughulisha na mafunzo ya walimu, wajibu ambao uko chini ya Idara ya Utathmini wa Ubora na Viwango (Directorate of Quality Assurance and Standards) katika wizara ya Elimu. Kufikia sasa TSC imewafundisha jumla ya walimu 218, 283 kuhusu mtaala wa CBC.