TSC kupandisha zaidi ya walimu 2,400 vyeo

TSC kupandisha zaidi ya walimu 2,400 vyeo

Na FAITH NYAMAI

TUME ya Huduma za Walimu Nchini (TSC), inapanga kuandaa mahojiano wiki hii ili kuwapandisha vyeo walimu 2,419 katika shule za msingi na upili nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TSC, mahojiano hayo yataanza mnamo Novemba 1, kisha yakamilike Novemba 12 katika kiwango cha maeneo na kaunti.

Mahojiano hayo pia yanatarajiwa kupandisha vyeo walimu wakuu na manaibu wao 1,376 wanaohudumu katika maeneo kame.

“Tumechukua hatua hii kuhakikisha kuwa walimu wanapandishwa vyeo kwenye taaluma hii ya ualimu. Mahojiano haya ni kulingana na mwongozo wa kuwapandisha walimu vyeo uliokumbatiwa mnamo 2018,” ikasema taarifa ya TSC.

Aidha mahojiano kwa walimu 1,995 ambao wamekuwa wakihudumu kupitia kandarasi, yatafanyika mwezi ujao pamoja na yale ya walimu 1,038 wa shule za msingi na 967 wa shule za upili.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, TSC imewapandisha vyeo zaidi ya walimu 100,000 kulingana na mkataba uliotiwa saini wa CBA mnamo 2017 ambao muda wake ulifikia tamati mnamo Juni 30, 2021.

Kati ya waliopandishwa vyeo ni walimu 15,407 ambao walihojiwa mnamo Disemba 2020 na Februari 2021. Jumla ya walimu 115,197 idadi inayojumuisha walimu wakuu, manaibu wao na walimu wengine, wamepandishwa vyeo mwaka huu.

“Kwa mujibu wa CBA, walimu wote ambao walikuwa wamehudumu kwa gredi moja ya kazi wanafaa wapandishwe vyeo,” ikaongeza taarifa ya TSC.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia akitangaza nafasi ambazo zinafaa ziwaniwe, alisema zitajazwa na walimu kupitia mahojiano ambayo yatakuwa na uwazi mkubwa na wale waliohitimu pekee ndio watapewa nafasi hizo.

Aidha alisema mpango wa kuwapandisha vyeo walimu wanaohudumu katika maeneo kame yenye mazingira magumu ya kufanya kazi unafaa kwa kuwa walimu wakuu na manaibu wao wamekuwa wakishikilia vyeo vyao kwa muda kwa miaka mitatu iliyopita.

Pia mahojiano haya yatasaidia kuongeza idadi ya walimu wanaohudumu maeneo kame baada ya wengi kuondoka mwaka jana kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama.

Pia TSC inapanga kurefusha kandarasi za walimu 4,005 walioajiriwa kwa mkataba kwa muda wa mwaka mmoja pekee.

Kufikia mwisho wa mwaka 2022, idadi ya walimu hao itakuwa imeongezeka hadi 6,000.

You can share this post!

Watford waduwaza Everton na kuvunia kocha Ranieri ushindi...

Ibrahimovic ajifunga kabla ya kuongoza AC Milan kuzamisha...

T L