TSC yaadhibu walimu wanaotoza karo zaidi

TSC yaadhibu walimu wanaotoza karo zaidi

Na FAITH NYAMAI

WIZARA ya Elimu imewasilisha kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) majina ya walimu wakuu wanaotoza wazazi karo zaidi ili wachukuliwe hatua.

Hatua hii inajiri huku tume hiyo ikimsimamisha kazi mwalimu mkuu wa shule ya wavulana ya Nakuru High, Yator Mike Kiplagat kwa kukiuka mwongozo wa serikali kuhusu karo.

Bw Yator alisimamishwa kazi kupitia barua aliyoandikiwa na Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti ya Nakuru, Fredrick Nganga.

“Ulitoza wanafunzi karo zaidi mwaka wa 2020 na 2021 kinyume na sehemu ya 29 ya sheria ya elimu msingi ukiwa mwalimu mkuu wa shule ya wavulana ya Nakuru Boys High school. Kufuatia hatua hiyo, umesimamishwa kazi kuanzia Septemba 1, 2021,” ilisema barua hiyo.

TSC pia imemuagiza mwalimu mkuu huyo kuandika taarifa ya kujitetea kwa tume ndani ya siku 21 na kumwalika kutoa ushahidi kuunga hatua yake.

Katibu wa Elimu ya Msingi Dkt Julius Jwan jana alisema wizara imekuwa ikikusanya habari kutoka shule kote nchini na imekuwa ikiwasilisha ripoti kwa TSC ichukue hatua.

Hata hivyo, hakufichua majina na idadi ya walimu ambao maelezo yao yamewasilishwa kwa TSC wachukuliwe hatua akiahidi kufanya hivyo mchakato wa kuwaadhibu ukikamilika.

Dkt Jwan alisema walianza kukusanya ripoti kuhusu walimu wakuu wanaokiuka mwongozo wa karo kuanzia Agosti na wataendelea kufanya hivyo.

“Kama wizara, tumetoa maagizo kwa walimu wakuu wa shule kufuata iwapo wanataka kutoza karo zaidi wanafaa kupata kibali kutoka kwetu,” alisema Dkt Jwan.

You can share this post!

Raila anyenyekea wazito Mlima Kenya

IEBC na Kihara wakata rufaa kunusuru BBI