Habari Mseto

TSC yaajiri walimu 8,000

September 3rd, 2018 1 min read

OUMA WANZALA Na PETER MBURU

Tume ya kuwaajiri walimu (TSC) imeanza kuwatuma shuleni zaidi ya walimu 8,000 ambao iliajiri, wakitarajiwa kuanza kuripoti madarasani Jumatatu. 

Walimu hao 8090 walioajiriwa wanatarajiwa kusaidia kutimiza lengo la serikali la kufanya kila mwanafunzi anayemaliza shule ya msingi aendelee na masomo ya shule ya upili.

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa TSC Nancy Macharia alisematayari walimu 7,817 wamepokea barua za kuwaajiri, huku 273 wakiwa wamehojiwa lakini wanasubiri barua baada ya kukosa vitu  vinavyohitajika.

“Jumla ya walimu 903 wamepokea barua za kuwaajiri kufunza shule za msingi, huku 6,914 wakiwa walimu wa shule za upili,” Bi Macharia akasema.

Walimu hao sasa wanatarajiwa kusuluhisha upungufu wa walimu katika shule za umma. TSC ilitangaza nafasi 8,700 za walimu na hadi sasa, nafasi 610 zinasalia wazi.

Hii ni baada ya tume hiyo kuitaka serikali kuipa Sh8.3bilioni kuajiri walimu 12,626 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mine, lakini serikali ikaipa Sh5bilioni.

Kulingana na takwimu za TSC, kuna takriban walimu 290,000 ambao wamepitia mafunzo lakini bado hawana ajira.

Tume hiyo aidha ilikuwa imeiomba wizara ya fedha kuipa Sh16bilioni kuajiri walimu wa kujifunza (interns) 68,000, kama njia ya kutoa suluhu ya muda mfupi.

“Kwa uhitaji wa walimu wa kujifunza, hatutahitaji kuajiri walimu kila mwaka kwani tutawaajiri wao pale nafasi zinapotokea kisha tunawaajiri wengine wa kujifunza,” akasema Bi Macharia.

Kulingana na maeneo, kaunti ya Bungo inaongoza kwa upungufu wa walimu, kwa walimu 3,523 ikifuatwa na Kakamega kwa kukosa walimu 3,422, Kitui-2,571 na Narok-2,162.

Kwa zile zilizojitosheleza, kaunti ya Isiolo inahitaji walimu 12 pekee, Lamu-44 na Nairobi 87 wa shule za msingi, akasema Bi Macharia.