Makala

SEKTA YA ELIMU: TSC yafaa kubuni sera thabiti ya uajiri wa walimu vibarua

October 9th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ya kuajiri walimu 10,300 vibarua imetajwa kama itakayoleta afueni kidogo katika shule za umma zinazokumbwa na uhaba mkubwa wa walimu.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya elimu na wadau wameitaka TSC kushughulikia mambo kadha ambayo wanasema huenda yakaathiri utendakazi wa walimu hao katika shule mbali mbali watakakotumwa kuhudumu.

Kulingana na mshirikishi wa Shirika la Uwezo Kenya, John Mugo ilifaa kuunda na kuchapisha rasmi sera ambayo itaongoza mpango mzima wa uajiri wa walimu hao ni miongoni mwa jumla ya walimu 328,324 waliohitimu lakini hawana ajira.

“Kunapasa kuwa na sera itakayotoa mwongozo kuhusu viwango vya mishahara, na marupurupu mengineyo, ambayo walimu kama hao watakuwa wakipokea katika kipindi mahsusi watakaohudumu. Vilevile, mipaka ya kazi yao itaweka wazi kwani haifai kuwa sawa na walimu wa kudumu,” anasema Dkt Mugo.

Mtaalamu huyo anahoji tangazo la TSC kwamba vibarua wataofundisha katika shule za msingi watalipwa mshahara wa Sh10,000 kila mwezi huku wenzao watakaofunza katika shule za upili watapokea Sh15,000 bila kujali mazingira watakaohudumu.

“Hamna mantiki ya kumtuma mtu aliyezaliwa na kulelewa katika tuseme kaunti ya Busia kwenda kufunza katika maeneo yenye mazingira magumu kama vile kaskazini mwa Kenya kwa mshahara wa Sh10, 000, ambazo baada ya kutozwa ushuru huenda zikasalia Sh8,000,” anasema.

Wakati huu mwalimu wa kudumu wa shule ya msingi mshahara wa Sh20, 000 kwa mwezi huku yule anayesomesha katika shule ya upili huanza kwa mshahara wa kima cha Sh32, 000, kabla ya kujumuishwa marupurupu.

Dkt Mugo anasema ingekuwa bora iwapo TSC ingewalipa walimu hao kulingana na kiwango cha ugumu wa maisha katika mazingira ambako watatumwa kuhudumu.

Kulingana na tangazo la TSC walimu hawa watatumwa katika shule yoyote nchini ambako kuna uhaba wa walimu. Hii ina maana kuwa huenda wengi wao wakatumwa kufanya kazi katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Kenya ambako kuna uhaba mkubwa wa walimu kufuatia visa vya mwaka 2018 ambapo walikuwa walimu wasio wenyeji walidhulumiwa.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta David Okello anasema huenda walimu hao wakakabiliwa na unyanyapaa wanafunzi wao wakibaini kuwa wao ni vibarua, wala sio walimu wa kudumu.

“Hali kama hii huwapata walimu vibarua ambao huajiriwa na bodi zinazosimamia shule mbali mbali kufidia uhaba wa walimu. Walimu wa kudumu pia huwachukulia wenzao vibarua kama wenye hadhi ya chini kuliko wao, hali ambayo inaweza kuathiri uwiano na utangamano miongoni mwa walimu japo wako na uhitimu sawa,” anasema Dkt Okello ambaye anafunza kozi ya Saikolojia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Nchini (Knut) anaunga mkono hatua ya TSC kuajiri walimu vibarua lakini anasisitiza kuwa sharti iwape ajira ya kudumu baada ya muda wao wa kuhudumu kukamilika.

“Knut inaunga mkono hatua hii japo idadi ya watakaoajiriwa ni ndogo zaidi kwani shule za msingi zina uhaba wa walimu 125,000 katika shule za msingi za umma huku zile za upili zikikosa walimu 95,000. Lakini TSC itoe hakikisho kwamba baada ya mwaka mmoja walimu hawa wote 10,300 watapewa ajira ya kudumu, bila ubaguzi,” anasema. Lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Dkt Nancy Macharia anasema baada ya mwaka mmoja kuisha ni wale waliodhihirisha utendakazi mzuri pekee ndio watapewa ajira rasmi.