Habari Mseto

TSC yamtetea mwalimu aliyekemea mwanafunzi kuhusu hedhi

September 22nd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TIME ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) huenda ikamwondolea lawama mwalimu aliyedai kumzomea mwanafunzi wa kike kwa kuchafua sare yake kwa damu ya hedhi, na kupelekea mwanafunzi huyo kujitia kitanzi.

Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Nancy Macharia alisema maafisa wake waliochunguza kicho cha mwanafunzi huyo Jackline Chepng’eno walibaini hakudhulumiwa mwalimu Jenniffer Chemutai ilivyodaiwa.

Marehemu ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa sita katika Shule ya Msingi ya Kabiangek iliyoko kaunti ndogo ya Konoin, Kaunti ya Bomet akijitoa kinyonga mnamo Septemba 6, 2019. Alijiua karibu na mto, ambako alienda kuteka maji ya kuonyesha sare yake, kwa kutumia leso.

“Mwalimu Mkuu, walimu na wanafunzi wa darasa la sita waliohojiwa na maafisa wetu waliambiwa kuwa Mwalimu Chemutai hakumdhulumu marehemu bali alijaribu kumsaidia kwa kumpa sodo. Lakini Jackline alikaidi ushauri huo na kufululiza hadi nyumbani,” Dkt Macharia akasema katika ripoti hiyo.

Na mamake marehemu, Bi Beatrice Kirui, pia alithibitisha kuwa alifika nyumbani na kusema ameagizwa kubadilisha mavazi kisha arejee shuleni.

Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu wanafunzi wa kike 50, waliobaleghe, walikuwa wamepewa sodo, mbili kila mmoja.

“Na wakati wa mkasa, maafisa wetu walibaini kuwa Shule ya Msingi ya Kibiangek ilisalia na sodo 77 za ziada,” ripoti hiyo ikasema.

Dkt Macharia alisema TSC imeamua kumpa likizo ya lazima mwalimu huyo (Bi Chemutai) kulinda usalama wake baada ya wanakijiji kutisha kumshambulia.

Aidha, tume hiyo ilichukua hatua hiyo ili kuipa nafasi ya kuendesha uchunguzi huru na wa kina ili kubaini ikiwa mwalimu huyo alikiuka kanuni zozote za kitaalum.

“Likizo hiyo pia itamhakikishia mwalimu huyo usalama wake kando na kumpa nafasi ya kujitetea dhidi ya madai yanayomkabili,” Dkt Macharia akaeleza.

Uchunguzi uliendeshwa na kundi la maafisa kutoka TSC na Idara ya Elimu ya Msingi. Wao ni Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti, Mkurugenzi wa TSC anayesimamia Kaunti hiyo ya Bomet, Afisa wa Kutathmini Ubora, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ndogo, Mkurugenzi wa TSC katika kaunti ndogo na Afisi anayesimamia masuala ya mtaala.

Kisa hicho kiliibua kero miongoni mwa wanakijiji walivamia shule hiyo wakitaka kumshambulia Mwalimu Chemutai.

Hata hivyo, walikabiliwa na maafisa wa polisi waliofaulu kuwatia mbaroni baadhi yao. Ghasia hizo zilipelekea kufungwa kwa shule hiyo kwa muda wa wiki mmoja ili kutuliza joto hilo.

TSC ilitoa ripoti hiyo kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Bomet Joyce Korir, akitaka taarifa kuhusu kilichosababisha kifo cha marehemu Chepngeno.