Habari Mseto

TSC yaonya walimu wakuu dhidi ya kuajiri waliofutwa

June 12th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imeapa kuwachukulia hatua kali walimu wakuu watakaoajiri walimu waliotolewa katika sajili ya tume hiyo kutokana na utovu wa nidhamu.

Akizungumza mjini Mombasa katika kongamano la walimu wakuu, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Dkt Nancy Macharia alisema walimu waliopokonywa nambari ya sajili ya tume hiyo kwa makosa ya kushiriki mapenzi na wanafunzi hawastahili kuruhusiwa kuingia darasani.

Aidha aliwaamrisha walimu wakuu kutoruhusu walimu ambao hawajasajiliwa na tume hiyo kufundisha ili kudhibiti visa vya TSC kuchafuliwa jina na wachache ambao hawatambuliki na tume hiyo.

“Tunatoa hatua hii wakati huu ambao tumekuwa tukishuhudia visa vya walimu kudhulumu wanafunzi kimapenzi, kisha tukinyooshewa vidole vya lawama kama waajiri wao. Hatutakubali kuchafuliwa jina na watu ambao hawatambuliki na tume,” alisema.

Ikiwa ni siku ya tatu tangu kongamano hilo kuanza mkurugenzi huyo alisema tume hiyo haitamuhurumia mwalimu yeyote atakayehusika kimapenzi na mwanafunzi licha ya umri wa mwanafunzi.

“Haijalishi mwanafunzi ana umri wa miaka mingapi hata kama ni miaka 30, kama bado yuko shuleni tutamlinda kutokana na walimu wanaokiuka sheria za ajira,” alisema Dkt Macharia.

Wakati huo huo amewakataza walimu dhidi ya kufuata maagizo kutoka kwa watu ambao yanakiuka sheria za tume hiyo.

Dkt Macharia amesema ni upuzi kwa walimu kutarajia kulipwa mshahara kutoka kwa tume ya ajira ilhali wanapokea maagizo kutoka kwa watu ambao hawana nia safi na tume hiyo.

“Inatuumiza moyo kila mara tunalazimika kuadhibu walimu ambao wamepotoshwa kwa kupewa maneno ya uchochezi ambayo si sahihi,”alisema.

Pia amewataka walimu wakuu kuhudhuria shuleni kila Siku na iwapo watakuwa na udhuru basi kujulisha tume mapema kuepuka malumbano.

“Sisi ni binadamu tunapatwa na matatizo hivyo mnaomba ruhusa,msipofanya hivyo msitarajie sisi kujitia hamnazo, tutawaandama na kukuadhibu kulingana na sheria,” alisema.