TSC yashtakiwa kukata ada walimu wasio vyamani

TSC yashtakiwa kukata ada walimu wasio vyamani

Na FAITH NYAMAI

WALIMU wawili wamewasilisha kesi kortini wakitaka Wizara ya Leba izuiwe kuidhinisha hatua ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kukata ada ya uanachama kutoka kwa mishahara ya walimu ambao si wanachama wa vyama vya kutetea maslahi ya walimu.

TSC ilitoa pendekezo hilo katika Mkataba wa Maelewano (CBA) ya mwaka wa 2021 hadi 2025 iliyotia saini pamoja na vyama vya kutetea maslahi ya walimu Julai.

Vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (Kuppet) na Chama cha Kutetea Maslahi ya Walimu wa Shule za Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum (Kusnet).

Katika stakabadhi zilizowasilishwa katika mahakama ya Kisumu, Bw Stephen Onditi na Bw Paul Nzyathyu pia wanataka TSC izuiliwe kutekeleza agizo hilo lililoidhinishwa na Wizara ya Leba.

Mbali na vyama hivyo vya kutetea maslahi ya walimu, TSC na Wizara ya Leba pia zimeorodheshwa kama washtakiwa.

“Hakuna ada za uanachama zitakazolipwa na walimu ambao si wanachama wa vyama vya kutetea maslahi ya walimu vilivyotajwa hapa; Knut, Kuppet na Kusnet,” ikasema sehemu ya stakabathi za kesi zilizowasilishwa mahakamani na walimu hao wawili.

Wanasema hatua hiyo ya Waziri wa Leba kuchapisha ada hiyo ya uanachama itawaathiri walimu wahusika kisaikolojia na kupunguza mapato yao. Kuppet hutoza ada ya uanachama ya asilimia 1.8 ya mshahara wa walimu, kila mwezi, Knut hutoza asilimia 2 huku Kusnet ikikata asilimia 1.45.

Ikiwa utozaji wa ada hiyo utatekelezwa jinsi ilivyoidhinishwa na Wizara ya Leba pamoja na vyama vya walimu zaidi ya walimu 190,000 katika shule za msingi na upili watahitajika kulipa ada hiyo ya uanachama kila mwezi.

You can share this post!

TAHARIRI: Mauaji ya vijana yatia hofu

Mhukumiwa aeleza jinsi walivyomuua naibu gavana