TSC yasifu walimu kujitolea kisiwani

TSC yasifu walimu kujitolea kisiwani

NA MAUREEN ONGALA

MWALIMU mkuu wa Shule ya Upili ya Marafiki iliyo katika Kisiwa cha Kadaina, Wadi ya Matsangoni, Kaunti ya Kilifi nusura aadhibiwe alipowasili katika kituo cha kuchukua karatasi za mitihani akiwa amevalia kaptura (kinyasa).

Mwalimu huyo mkuu alikuwa amefika katika kituo hicho ambapo shughuli ya kufungua karatasi za mitihani ilikuwa inasimamiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Bi Nancy Macharia.

“Nilidhani hakuwa mtu ambaye alifaa kuwa hapo kwa sababu sitarajii mwalimu awe amevaa kinyasa. Alinieleza ilikuwa ni kwa vile lazima atembee ndani ya maji kabla afikie boti inayomleta hapa,” akasema Bi Macharia, jana Jumatatu.

Bi Macharia aliamua kuzuru shule hiyo iliyo katika eneobunge la Kilifi Kaskazini jana Jumatatu ili ajionee mwenyewe masaibu ambayo walimu na wanafunzi hupitia kila siku, ambapo pia alikagua jinsi Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) unavyoendelea.

Shule ya Msingi na Upili ya Marafiki iko katika eneo ambapo walimu na wanafunzi lazima wavuke Bahari Hindi kwa boti ili kuifikia.Kulingana na Bw King’oo, changamoto ya usafiri imeathiri sana shule hiyo kwa kiasi cha kuwa walimu wengi huwa hawataki kuajiriwa hapo.

“Imekuwa changamoto ya muda mrefu kwetu. Hatuwezi kufanya mahojiano ya wafanyakazi katika shule hii kwa sababu hakuna mtu atakayekubali kuja hapa. Wale wanaoajiriwa na Bodi ya Usimamizi wa shule huwa hawakai zaidi ya miezi mitatu,” akaeleza.

Kwa sasa, shule ya upili ina walimu wanane pekee walioajiriwa na TSC ilhali walimu 11 zaidi wanahitajika.

Bw King’oo alieleza kuwa maboti huwa hayawezi kubeba watu wengi kwa safari moja kwa hivyo wakati mwingi walimu na wanafunzi huchelewa kwani lazima wasubiri boti ambayo hupeleka watu kisha irudi kuwachukua.

“Tumefurahi kuwa sasa Bi Macharia ameandamana nasi hadi shuleni akajionea changamoto ambazo huwa tunapitia. Tuna matumaini atawasilisha masaibu yetu kwa wenzake ili nasi pia tuzingatiwe kupokea marupurupu ya kufanya kazi katika hali ngumu,” akasema.

Mara kwa mara, huwa kuna mawimbi makali ambayo hutatiza zaidi safari za kuenda shuleni mbali na kuhatarisha maisha yao.

Aliongeza kuwa wanaendeleza mipango ya kujenga ukuta wa kuzunguka shule hiyo ili kuzuia maji kuwafikia shuleni wakati mawimbi yanapozidi.

“Mawimbi makuu huwa yanatatiza masomo yetu ya zaidi asubuhi kwa sababu ni lazima walimu na wanafunzi wasubiri hadi yatulie ndipo wapate nafasi ya kutembea ndani ya maji wakija shuleni baada ya kushuka kwenye boti,” akasema.

TSC imewasifu walimu wanaohudumia shule hiyo kwa kujitolea kwao licha ya hali ngumu wanayopitia kila siku.

Bi Macharia alisema safari yake ya kufika katika shule hiyo imempa taswira halisi ya jinsi hali ilivyo.

“Tumejionea kile ambacho walimu hupitia wanapokuwa kazini. Wanasafiri kwa barabara kwa zaidi ya nusu saa, kisha wanatembea ndani ya maji kabla kufikia boti na kutumia dakika nyingine 45 kufika shuleni,” akasema.

Alieleza kuwa huwa ni vyema maafisa wakuu serikalini kujua jinsi wafanyakazi wanavyotekeleza majukumu yao.

“Kwa kweli ni safari ndefu na si rahisi kusafiri kila siku kuziendea karatasi za mitihani kisha kurudisha tena karatasi hizo baada ya mitihani kukamilika,” akasema.

Shule ya Upili ya Marafiki ina jumla ya wanafunzi 204, ambao ni ongezeko ikilinganishwa na 168 waliokuwa wakisoma hapo Februari 2021.

Afisa Mkuu wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Nancy Macharia pamoja na maafisa wengine wa tume hiyo wakiwa kwenye boti ndani ya Bahari Hindi wakielekea katika Shule ya Upili ya Marafiki katika kisiwa cha Midoina, Matsangoni, Kilifi Kaskazini, Desemba 05, 2022. PICHA | MAUREEN ONGALA

Kuna watahiniwa 50 wa KCSE katika shule hiyo ambapo 23 ni wavulana na 27 ni wasichana.

Watahiniwa hao jana Jumatatu walianza mitihani yao saa tatu asubuhi.

Karatasi hizo za mitihani jana Jumatatu zilifunguliwa katika afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, dakika 20 kabla ya saa moja asubuhi.

Afisa Mkuu wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Nancy Macharia (kushoto) akiwa amebeba viatu akiwa pamoja na maafisa wengine wa tume hiyo wakielekea katika Shule ya Upili ya Marafiki katika kisiwa cha Midoina, Matsangoni, Kilifi Kaskazini, Desemba 05, 2022. PICHA | MAUREEN ONGALA

Bi Macharia alianza kwa kuwahutubia walimu wakuu kisha kufungua karatasi hizo saa moja kamili.Alitoa wito kwa walimu wote nchini kuhakikisha hakutakuwa na udanganyifu katika mtihani huo.

“Singependa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mwalimu yeyote. Kusiwe na visa vya udanganyifu wala ulaji rushwa. Achene wanafunzi wapate matokeo wanayoweza kupata ili wafanye yale ambayo wamepangiwa na Mungu,” akasema Bi Macharia.

Alikuwa ameandamana na Mkurugenzi wa TSC eneo la Pwani, Victoria Muoka, Mkurugenzi wa TSC Kilifi, Lesayo Megirin, na Naibu Kamishna wa Kaunti wa Kilifi Kaskazini, Bw Andrew Tanui.

  • Tags

You can share this post!

Cherera naye ajiuzulu na kuacha Raila hoi

Klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia yaweka mezani Sh25.8...

T L