WYCLIFFE NYABERI NA RUTH MBULA
WALIMU sita walionaswa kwenye video wakiwalazimisha watoto wadogo wavulana kufanya maigizo ya ngono wamesimamishwa kazi kwa muda.
Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iliwapa barua zao punde baada ya kufikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Ogembo Paul Biwott.
Ingawa hawakushtakiwa rasmi kortini, TSC katika barua iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji Mkuu wake E. J Mitei, iliwajulisha kuwa wamesimamishwa kazi na waonyeshe sababu kwa nini hawafai kutolewa kwenye sajili ya walimu.
Barua hizo zilitumwa kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi Evelyne Moraa Orina, Catherine Mokera Mokaya, William Isuka, Druscilla Moraa Nyairo, Angellica Joseph na Gladys Kenyanya.
Bw Obadiah Nyaribo Mokaya ambaye pia alifikishwa kortini na wenzake sita hata hivyo hajaorodheshwa na TSC. Saba hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Nyangusu hadi leo Ijumaa saa tatu asubuhi watakapojua hatima yao.