Habari Mseto

TSC yatangaza mwongozo mpya wa ajira

May 22nd, 2018 2 min read

Na FAITH NYAMAI

WALIMU wapya katika shule za msingi watahitajika kuandika barua ya kujitolea kutumikia kwa angalau miaka mitano katika kaunti watakakoajiriwa kabla ya kuomba kuhamishwa katika kaunti nyingine.

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilitoa mwongozo huo Jumatatu huku ikitaka kutatua uhaba uliopo katika shule mbalimbali nchini hasa katika eneo la Kaskazini Mashariki.

Wiki iliyopita TSC ilitangaza nafasi za kazi za walimu 8,672 kote nchini.

Miongoni mwao, 7,672 watahitajika kufunza katika shule za upili huku 1,000 wakitakikana kufunza katika shule za msingi.

Mwongozo huo mpya umetolewa wakati ambapo walimu wamekuwa wakitoroka kaunti za Kaskazini Mashariki za Mandera, Garissa na Wajir kutokana na ukosefu wa usalama.

Kumekuwa pia na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Kaskazini Mashariki wanaotaka serikali iajiri wa wa jamii za eneo hilo kuwa walimu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia, alisema wote watakaoomba kazi watahitajika wawe wamesajiliwa na tume hiyo.

Mahitaji hayo mazito yanatarajiwa kuvutia ukosoaji kutoka kwa walimu ambao wamekuwa wakipinga kuajiriwa kwa walimu maeneo ya mbali kutoka kaunti zao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Wilson Sossion amekuwa akipinga kuajiriwa kwa walimu katika kaunti ambazo hazina usalama.

Mnamo Machi, TSC ilihamisha walimu 1,000 kutoka kaunti za Kaskazini Mashariki baada ya mamia ya walimu kukita kambi katika makao makuu ya tume hiyo kutaka wahamishwe.

Kwenye mwongozo mpya, wakurugenzi wa TSC katika kaunti watahitajika kufunza wanachama wa baraza litakalofanya mahojiano kuhusu mwongozo wa sheria kabla shughuli ya kuajiri walimu wapya ianze.

 

Mabaraza

Wakurugenzi wa TSC katika kaunti ndogo watahitajika kubuni baraza litakalojumuisha afisa anayesimamia wafanyakazi wa TSC katika kaunti ndogo ambaye atakuwa katibu wa baraza hilo, na maafisa wote wa usaidizi wa mtaala katika maeneo ya kaunti ndogo watakuwa wanachama.

Mabaraza hayo yatahitajika kuchagua watu wanaotaka kuajiriwa kuwa walimu na kuwasilisha orodha ya watakaopita mahojiano kwa baraza la uajiri la kaunti, na baadaye orodha itapelekwa kwa makao makuu ya TSC.

Bi Macharia alisema wale ambao hawajasajiliwa na tume hiyo lazima waambataniishe vyeti vya kuthibitisha wametuma ombi ya kusajiliwa, kwenye barua zao za kuomba kazi.

Wale ambao wamewahi kuajiriwa kama walimu watahitajika kuandika nambari zao za usajili wa TSC na kueleza kwa nini waliacha kazi.

Hata hivyo, Bi Macharia alisema watazingatia zaidi kuajiri watu ambao hawajawahi kuajiriwa na TSC.

Tume hiyo pia imetoa nafasi kwa wafanyakazi wa idara nyingine za serikali wawasilishe maombi kama wana matakwa yanayohitajika.