TSC yatuza shule, walimu waliofana zaidi masomoni

TSC yatuza shule, walimu waliofana zaidi masomoni

Na FAITH NYAMAI

WALIMU wakuu na walimu ambao wanafunzi wao walifanya vyema katika mitihani ya kitaifa ya shule za upili na msingi mwaka 2020, Jumanne walituzwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu TSC, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani.

Walimu 31 walituzwa katika makundi mbalimbali ambayo TSC ilitambua kung’aa kwao hasa katika kutoa mafunzo, usimamizi na utekelezaji faafu wa mtaala kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia, Jumanne alisema mchakato wa kuwatambua walimu hao ulikuwa na uwazi na hasa ulizingatia utendakazi wao pamoja na maadili yao kazini kulinga na sera za Wizara ya Elimu.

“Walimu hao 31 watatuzwa kulingana na sera za wizara na pia kanuni za TSC ambazo zinasisitizia uwajibikaji na utambulizi,” akasema Bi Macharia.

Kati ya waliotambuliwa na kutuzwa ni Walimu Wakuu Sammy Kipchumba (Kapsabet Boys), Florah Mulatya (Kenya High), John Munyua (Mangu High), William Macharia (Alliance High, Kiambu) na Jacinta Njeri (Mary Hills).

Pia walimu wakuu wa shule za msingi hawakuachwa nyuma baada ya shule zao kufanya vyema katika mtihani wa KCPE.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Utafiti, Kaunti ya Makueni Stephen Ngoma aliongoza orodha ya waliotuzwa.

Wengine ni Josleen Karimi (Kathigifiri, Meru), Anne Onyancha (St Peter’s Mumias, Kakamega), Charles Kimutai (Tenwek, Bomet), Isaac Magut (St Mathews Septonok) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nandi Hills Jerotich Getrude.

Vitengo vingine vilivyotuzwa ni shule tano za msingi na upili zilizoimarika katika matokeo ya mwaka 2020.

Pia shule tano spesheli zilizopata matokeo bora na walimu wakuu wa shule zilizotoa wanafunzi walioongoza kwenye KCPE na KCSE.

Pia Mwalimu Bora Duniani 2018 Peter Tabichi wa Shule ya Mseto ya Keriko, Eric Ademba wa Asumbi Girls aliyeshinda tuzo ya Mwalimu Bora wa Muungano wa Afrika (2019) kisha mshindi wa tuzo hiyo 2020 Jane Kimiti wa Othaya Girls, Kaunti ya Nyeri pia walituzwa na TSC Jumanne.

Tuzo za Jumanne zilikuwa za kwanza ambazo TSC imetoa kwa walimu huku Bi Macharia akieleza kwamba tume hiyo itaendelea kuwazawidi walimu wanaojituma na kuhakikisha wanafunzi wao wameng’aa kwenye mitihani na nyanja mbalimbali.

Mada ya mwaka huu 2021 ilikuwa ‘Walimu ndio kitovu cha kuboresha na kufufua Ualimu’.

Waziri Msaidizi wa Elimu Dkt Sarah Ruto naye alisema ualimu ni kazi ambayo inahitaji kujituma na akawashukuru walimu wanaojitolea kuhakikisha wanafunzi wao wameelimika.

“Tujikaze ili kuifanya taaluma hii iheshimiwe nao wanafunzi wetu wanufaike,” akasema Dkt Ruto.

Sherehe za jana zilishirikisha vyama vyote vya kutetea maslahi ya walimu KNUT, KUPPET na KUSNET.

Pia Miungano ya Walimu Wakuu wa Shule za upili (KESSHA), msingi (KEPSHA) na ule wa walimu wanawake (KEWOTA) walihudhuria sherehe hizo.

“Walimu wamekuwa wavumilivu na wameonyesha ukakamavu hasa wakati huu wa janga la corona. Serikali inafaa iwape ajira zaidi na kuwaongeza mishahara,” akasema Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori.

You can share this post!

Benki ya NCBA yazindua tawi la Ruiru

Vilio serikali inunue mifugo iliyo hatarini