Tsunami yatikisa ndoa ya OKA

Tsunami yatikisa ndoa ya OKA

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa One Kenya Alliance (OKA) umekumbwa na mashaka yanayoweza kuufanya upasuke na kusambaratika hata kabla ya kusajiliwa kisheria katika afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Kufikia sasa, OKA ni pendekezo tu la kusuka muungano japo vinara wake wamekuwa wakifanya kampeni za kuuvumisha pamoja. Hii ni licha ya kukosekana kwa mkataba wa kuwaunganisha rasmi kupitia kwa msajili wa vyama vya kisiasa.

Mashaka ya OKA yanafuatia madai ya kuibuka kwa mirengo miwili miongoni mwa vinara wanne wa muungano huo uliobuniwa mnamo Machi 25, 2021.

Japo mara kadhaa vinara wa OKA; Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Gideon Moi (Kanu) na aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo (UDP) wamekuwa wakiendesha kampeni zao pamoja, duru zinasema kuwa kuna kambi mbili zinazovutana.

Seneta Moi na Bw Musyoka tayari wameonyesha dalili za kuegemea upande wa kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga ambaye anaonekana kupendelewa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake 2022.

Bw Jirongo, aidha ameonekana kuegemea mrengo huu kwani amejitokeza kuwa mkosoaji mkuu wa Dkt Ruto.

Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wameonekana kuanza kuegemea upande wa Dkt Ruto baada ya madai kuibuka kuwa kuna baadhi ya wabunge wa vyama vyao ambao ni washirika wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Hii ni licha ya kwamba Bw Mudavadi ameshikilia kikiki kuwa atakuwa debeni kivyake ikiwa OKA itafeli kuteua mgombeaji mmoja wa urais.

Hata hivyo, Naibu Kiongozi wa ANC, Bw Ayub Savula amekana madai kuwa Bw Mudavadi anapania kushirikiana na Dkt Ruto, akisema “hizo ni porojo zinazotolewa na wabunge ambao hupokea Sh50,000 kila mmoja kila wiki ili kuchora taswira kuwa ANC inaelekea kujiunga na UDA”.

Seneta Moi na Bw Musyoka wameonyesha kuwa wanamuunga mkono Bw Odinga baada ya kumwalika waziri huyo mkuu wa zamani katika mikutano ya wajumbe wa vyama vyao, hatua ambayo iliwakera wandani wa Mudavadi.

Kwa mfano, mnamo Oktoba 1, mwaka huu Bw Odinga alialikwa kama mgeni wa heshima katika Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) wa Kanu ambapo seneta huyo wa Baringo aliidhinishwa kuwa mgombeaji wa urais wa chama hicho.

Vilevile, Alhamisi wiki jana, Bw Musyoka alimwalika Bw Odinga katika NDC ya Wiper ambapo, ilivyotarajiwa, Musyoka aliiteuliwa rasmi kuwa mgombeaji wa urais.

Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Mudavadi, alikosoa hatua ya Musyoka kumwalika Bw Odinga katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Seneta Moi ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alikariri imani yake kwamba hatimaye wao kama OKA watashirikiana na Bw Odinga “kulikomboa taifa hili kutoka kwa viongozi fisadi”.

Wiki jana, Bw Malala na wabunge Titus Khamala (Lurambi) na Tindi Mwale (Butere) walimtaja Seneta Moi kama chanzo cha migawanyiko ndani ya OKA kwa kujisogeza karibu na Bw Odinga.

Wakihutubia wafuasi wao katika eneo la Matunda, Kaunti ya Kakamega, watatu hao walitoa makataa ya hadi Desemba 25, kwa vinara wa OKA kumtaja mgombea urais la sivyo ANC ijiondoe kutoka muungano huo.

“Tunawaambia wenzetu katika OKA kwamba tunataka kujua mgombeaji urais wa muungano huo kabla ya Desemba 25. Ikiwa mgombeaji huyo, ambaye tunajua ni Musalia Mudavadi, hatatajwa basi sisi kama ANC tutaondoka ili tuunde muungano mwingine utakaomwezesha Musalia kupata urais,” Bw Mwale akasema.

Mnamo Ijumaa Bw Musyoka aliwaambia washirika wa Bw Mudavadi katika ANC wakome kuwapa vinara wa OKA makataa ya kutaja mgombea wa urais na akawasuta kwa kumwalika Bw Odinga katika NDC ya Wiper.

Wadadisi wa siasa wanasema hizi ni dalili kwamba OKA imejaa mashaka, kushukiana na kuumbuana.

You can share this post!

Vigogo wapasua kura

Washirika wa Ruto wadai Obado avuruga chama cha Naibu Rais

T L