Michezo

Tuchel awashangaa mashabiki wa Man U kumzomea Di Maria baada ya kichapo

February 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Paris Saint Germain Thomas Tuchel amekiri kushangazwa kwake na kisa cha kuzomewa kwa winga wa timu hiyo Angel Di Maria na mashabiki wa Manchester United wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza ya kuwania Klabu Bingwa Barani Uropa Jumanne Februari 13 ugani Old Trafford.

Tuchel hata hivyo amesifu Di Maria kwa kuvumilia mashabiki hao na kuchangia ushindi wa 2-0 dhidi ya wapinzani wao usiku huo. Mabao haya yalifungwa na Presnel Kimpembe na Kylian Mbappe katika kipindi cha pili cha mchuano huo.

“Mimi nilifikiria kwamba alikuwa na mlahaka mwema na mashabiki lakini namshukuru kwa kuvumilia na kufanya vizuri kuchangia ushindi wetu. Kona hatari alizochanja pamoja na pasi za uhakika haswa katika kipindi cha pili zilitusadia kufunga bao la pili kupitia Kylian Mbappe,” akasema Tuchel.

Winger huyo raia wa Argentina anakumbukwa kwa kusakatia Manchester United msimu wa 2014-15 alikoshutumiwa vikali na mashabiki kwa kuonyesha kiwango duni cha mchezo ilhali alinunuliwa kwa bei ghali kutoka Real Madrid msimu uliotangulia.

Ushindi wa PSG ulikolezwa hata zaidi na kukosa kwa nyota wake Neymar, Edinson Cavani na Thomas Meunier.

“Hatukuwa na wachezaji wetu muhimu kikosini lakini timu ilionyesha ukomavu na kiwango cha juu cha soka. Nakiri kwamba huwa tuko bora zaidi ikiwa wamepangwa kikosini japo katika mchezo wa soka kila mchezaji ni muhimu na tulithibitisha hilo kwa kuwabamiza Manchester United nyumbani kwao,” akasema kiungo wa PSG Julian Draxler.