Habari Mseto

Tuju aonya viongozi fisadi ndani ya Jubilee

December 29th, 2019 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG’

CHAMA cha Jubilee kimetangaza kwamba kitawafungia nje viongozi wanaohusishwa na doa la ufisadi huku kikitarajiwa kuandaa uchaguzi wake mwaka ujao wa 2020.

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Jumamosi njia pekee ya kuhakikisha vita dhidi ya ufisadi vinaendelezwa jinsi alivyoamrisha Rais Uhuru Kenyatta ni kuhakikisha kwamba washikilizi wa nyadhifa mbalimbali chamani ni watu wasiohusishwa na sakata yoyote ya ufisadi.

Akishiriki mahojiano na ‘Taifa Jumapili’ nyumbani kwake Asembo, eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya, Bw Tuju pia alisema katiba ya chama hicho haivumilii wafisadi na wanachama ambao wanashiriki uozo huo hawatapewa nafasi ya kuwania au kushikilia cheo chochote.

“Huwezi kutetea ufisadi kisha useme wewe ni mwanachama wa Jubilee ilhali manifesto ya chama inaharamisha ufisadi,” akasema Bw Tuju.

Kwa sasa viongozi mashuhuri ndani ya Jubilee wanaendelea kuchunguzwa kuhusiana na sakata mbalimbali za ufisadi na tangazo la Bw Tuju huenda ikazima nia ya baadhi yao ya kuwania vyeo mbalimbali.

Baadhi ya magavana wa Jubilee wanaokabiliwa na ufisadi ni Ferdinand Waititu(Kiambu), Moses Lenolkulal(Samburu) na Mike Mbuvi Sonko(Nairobi).

Wabunge wengi wa Jubilee pia wanakabiliwa na kesi za ufisadi na usemi wa katibu huyo mkuu huenda ikazima ndoto zao za kuwa maafisa wa chama hicho kubwa zaidi nchini.

Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama anachunguzwa kuhusiana na kukwepa kulipa ushuru unaohusisha zaidi ya Sh400 milioni. Mwenzake wa Embakasi Kaskazini James Gakuya naye ameshtakiwa kwa kupokea Sh40 milioni kutoka kwa Hazina ya Kifedha ya Maeneobunge(CDF) kwa kutoa kandarasi za ujenzi wa barabara bila kufuata sheria.

Wabunge Alfred Keter (Nandi Hills), John Waluke (Sirisia), Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi), Ali Rasso (Saku) na Moses Kuria wa Gatundu Kusini pia wanakabiliwa na kesi za ufisadi.

Bw Keter anakabiliwa na kesi ya kughushi stakabadhi na kupokea Sh633 milioni, Bw Arama anakabiliwa na kesi ya kunyakua ardhi ya manispaa ya Nakuru huku Bw Kuria na Bw Rasso wakiwa na kesi za kutoa matamshi ya kueneza chuki.

Bw Rasso anadaiwa kuchochea ghasia kati ya jamii za Borana na Gabra katika Kaunti ya Marsabit huku Bw Kuria akitoa matamshi ya kuzua chuki kisiasa.

Chama cha kitaifa

Aidha Bw Tuju alisema chama hicho ni cha kitaifa kitahakikisha kuna usawa wa kieneo na uwakilishi wa jamii zote kubwa na ndogo nchini wakati wa uchaguzi wake.

Mbunge huyo wa zamani wa Rarieda pia alifichua kwamba Jubilee itajigatua na itakuwa na mshikilizi wa afisi zake katika kila kaunti hata zile ambazo ni ngome za vyama vya upinzani.

“Kwa mujibu wa katiba yetu, chama chetu kina matawi katika magatuzi 47. Lazima uwepo wetu uhisiwe katika kaunti zote kwa mfano Kilifi ambapo chama cha ODM kilishinda viti vyote kuanzia udiwani hadi ubunge. Wajumbe wa jubilee katika eneo hilo pia watakuwa wanathaminiwa jinsi walivyo wenzao kutoka Kiambu ambayo ni ngome ya chama,” akasema Bw Tuju.