Tukipunguza bei ya mafuta tutalemewa kufadhili shughuli za serikali – Wizara ya Fedha

Tukipunguza bei ya mafuta tutalemewa kufadhili shughuli za serikali – Wizara ya Fedha

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wataendelea kubebeshwa mzigo mzito wa bei za juu za bidhaa za mafuta baada ya serikali kukataa kupunguza ushuru na ada zinazotozwa bidhaa hiyo.

Katibu katika Wizara ya Fedha Julius Muia Jumatano aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kwamba hatua kama hiyo itaathiri uwezo wa serikali kufadhili bajeti yake ya sasa ya kiwango cha Sh3.3 trilioni.

“Kupunguzwa kwa ushuru unatozwa mafuta kutapunguza mapato ya serikali na hivyo kushindwa kufadhili shughuli zake ilivyoratibiwa katika bajeti ya mwaka huu. Hatua hiyo pia itachangia serikali kukopa zaidi hali itakayoleta madhara makubwa kwa uchumi na wananchi,” Bw Muia akaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Gladys Wanga.

“Kupunguzwa kwa ushuru huo pia kutaathiri muunda wa Sheria ya Ugavi wa Fedha baina ya Serikali Kuu na serikali za kaunti. Vile vile, tunahitaji fedha za kufadhili miradi kama vile ujenzi wa barabara, SGR miongoni mwa miradi mingine,” akaongeza.

Bw Muia alieleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta wakati huu kumechangiwa pakubwa na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.

“Hali hii imechangiwa na kupungua kwa uzalishaji wa mafuta na kupanda kwa hitaji lake baada ya mataifa mengine kuanza kuanza kufufua chumi zao zilizoathiriwa na ugonjwa wa Covid-19,” akasema.

You can share this post!

Wabunge wakiri IEBC imepungukiwa na fedha za uchaguzi

Uefa yakunja mkia kuadhibu Barcelona, Real Madrid na...