Michezo

Tukishinda mechi zilizosalia tutaibuka mabingwa EPL – Salah

April 16th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Liverpool Mohamed Salah amesema timu hiyo inahitaji ushindi katika mechi zake nne zilizosalia za Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) ili kutwaa ubingwa msimu huu wa 2018/19.

“Tunahitaji kushinda mechi zetu zote zilizosalia na kuomba Manchester City wateleze ikizingatiwa taji hili ni muhimu sana kwetu. Hata hivyo hatufai kupoteza dira tunapofuatilia matokeo yao kwa kuwa ushindi ndio muhimu sana kwetu,” akasema Salah ambaye pamoja na Sergio Aguero wanaongoza orodha ya wafungaji bora wa EPL kwa mabao 19.

Vijana wa kocha Jurgen Klopp walirejea kileleni mwa msimamo wa jedwali la EPL baada ya kushinda Chelsea 2-0 ugani Anfield Jumapili Aprili 14.

Mabao ya Salah na Sadio Mane yalihakikishia Liverpool alama zote tatu na pia kuwawezesha kukita kambi kileleni kwa alama 84, alama mbili mbele ya nambari mbili Manchester City ambao bado wana mchuano mmoja wa kuwajibikia.

Awali, Manchester City waliwaduwaza Crystal Palace 3-1 huku mechi kali dhidi ya watani wao wa jadi Manchester United ikiwasubiri ugani Old Trafford Aprili 24.

The Reds wanaonekana kusalia na mechi rahisi ikilinganishwa Manchester City msimu ukielekea kufika ukingoni. Watacheza dhidi ya Huddersfield Town na Wolves ugani Anfield huku mtihani mkali ukiwasubiri ugenini dhidi ya Newcastle na Cardiff City.