HabariSiasa

TUKO PAMOJA: Uhuru na Raila walikutana baada ya mashauriano ya kisiri

March 11th, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

Kwa ufupi:

  • Mkutano huo ulikuwa kilele cha msururu wa mashauriano ya kisiri ambayo yamekuwa yakiendelea kwa lengo la kuwaleta pamoja viongozi hao 
  • Mkutano  kati yangu na ndugu Raila utasaidia kutuliza joto la kisiasa lililotokana na uchaguzi wenye ushindani mkali – Rais Kenyatta
  • Wakenya wanataka mabadiliko na hayawezi kupatikana bila amani, umoja na haki. Wakati wa kufanya hivyo ni sasa  –  Odinga
  • Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula wakiri kuwa hawakuwa na habari zozote kuhusu mkutano huo

HATIMAYE Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga Ijumaa waliweka kando tofauti zao za kisiasa na kutangaza kufanya kazi pamoja kuunganisha Wakenya kwa ajili ya maendeleo.

Wawili hao walitangaza hayo walipohutubia wanahabari baada ya kufanya mashauriano ya masaa mawili katika Afisi ya Rais iliyoko jumba la Harambee jijini Nairobi.

Duru zilisema mkutano huo ulikuwa kilele cha msururu wa mashauriano ya kisiri ambayo yamekuwa yakiendelea kwa lengo la kuwaleta pamoja viongozi hao wawili.

Bw Odinga ambaye alikuwa wa kwanza kuwahutubia wanahabari alisema: “Hatufai kuruhusu kuwepo kwa mgawanyiko katika nchi hii kwa sababu ya tofauti za kisiasa. Hii ndio maana leo tumeamua kuweka kando tofauti zote za kikabila na kisiasa,” akasema Bw Odinga.

“Tumetoka mbali na hatuwezi kufika tuendako tukiwa tumegawanyika,” akasema.

Bw Odinga alisema japo Kenya ina Katiba mpya ambayo ilileta mageuzi katika mfumo wa uongozi kupitia kubuniwa kwa asasi mbali mbali za utawala, chaguzi bado zinaleta mgawanyiko nchini.

“Wakenya wanataka mabadiliko na mabadiliko hayo hayawezi kupatikana ikiwa hatulenga kupalilia amani, umoja na haki. Wakati wa kufanya hivyo ni sasa,” Bw Odinga akasema.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alitaja mkutano kati yake na Bw Odinga kama nafasi bora kwa wao kama viongozi kuanza kujadili masuala yenye umuhimu kwa taifa.

Rais Kenyatta pamoja na Raila Odinga walipokutana katika Harambee House, Nairobi ambapo walitangaza kusitisha uhasama kwa manufaa ya ustawi wa nchi. Picha/Hisani

Mwanzo mpya

“Huu ni mwanzo mpya. Mkutano  kati yangu na ndugu Raila utasaidia kutuliza joto la kisiasa lililotokana na uchaguzi wenye ushindani mkali na ambao ulisababisha migawanyiko nchini,” akasema Rais Kenyatta.

“Tunaweza kutofautiana kisiasa lakini sharti tuungane katika masuala yanayowaathiri Wakenya,” akaeleza.

Mshauri wa Bw Odinga Joseph Simekha jana alifichua kuwa kiongozi huyo aliamua kufanya kikao na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuhisi kusalitiwa na wenzake waliokwepa sherehe ya kuapishwa kwake Januari 30.

“Bw Odinga amebadili msimamo wa kuendelea kupinga serikali ya Jubilee baada ya kuhisi kusalitiwa na wenzake watatu waliokosa kufika Uhuru Park, Nairobi wakati wa sherehe ya kuapishwa kwake na badala yake wameanza kulenga uchaguzi mkuu wa 2022.

Na matamshi yao pia yameonyesha kuwa walikuwa wakimezea mate nyadhifa kubwa serikali wala sio kuendeleza ajenda ya mageuzi,” akasema Bw Simekha ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Alikuwa akirejelea kiongozi wa ANC Bw Mudavadi, mwenzake Wetang’ula na Bw Musyoka.

Hata hivyo, Bw Simekha alisema kuwa muungano wa NASA bado utaendelea kudumu hata baada ya mkutano wa jana kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

 

Hawakuwa na habari 

Hii ni licha ya Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula kukiri kuwa hawakuwa na habari zozote kuhusu mkutano huo wa Bw Odinga na Rais Kenyatta. Duru ziliambia ‘Taifa Leo’ kwamba, mkutano kati ya wawili hao ulipangwa kisiri bila kuwahusisha wandani wa karibu wa viongozi hao.

“Niliitwa na Baba (Raila) asubuhi na akanishauri kuvalia nadhifu tayari kwa shughuli fulani.

Aliniambia niandamane na msafara wake na ndipo nikajipata hapa katika jumba la Harambee kwa mkutano na Uhuru,” akasema Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed aliyehudhuria mkutano huo. Hata hivyo, mbunge huyo ambaye ni kiranja wa wachache bunge alidinda kutufichuliwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo.

Ujumbe wa Bw Odinga pia ulijumuisha bintiye Winnie Odinga na msemaji wake Denis Onyango.

Mkutano huo pia unajiri miezi miwili baada ya Bw Odinga kuapishwa kama “Rais wa Wananchi” katika hafla iliyoandaliwa katika bustani ya Uhuru, Nairobi, shughuli iliyosusiwa na vinara wenzake.