Habari za Kitaifa

Tuko sawa bila Raila, Kalonzo asema

February 19th, 2024 2 min read

Na CECIL ODONGO

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka jana alisema kuwa muungano wa Azimio la Umoja utasalia imara na kuendelea kutekeleza majukumu yake hata kama kinara wa Upinzani Raila Odinga hatashiriki siasa za Kenya.

Bw Musyoka alisema kuwa hakutakuwa na pengo lolote katika siasa za upinzani huku Bw Odinga ambaye amekuwa ‘sura’ ya Azimio akijiandaa kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Wiki jana, waziri huyo mkuu wa zamani akiwa ameandamana na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, alitangaza kuwa anataka kazi hiyo ya AUC. Muhula wa kudumu kwa mwenyekiti wa sasa wa AUC, Moussa Faki wa Chad, unatamatika Janauri 2025.

“Raila anaelekea kushikilia wadhifa wa juu na tunamwombea afanikiwe. Hapa tunaangalia maslahi ya Kenya au Azimio kwa sababu Raila sasa amekwea ngazi kutoka siasa za Kenya,” akasema Bw Musyoka.

“Ninawahakikishia kuwa sisi kama Azimio la Umoja tuko pamoja. Siku mbili baada ya Raila kutangaza azma yake, tulikutana na kukubaliana kuwa lazima Azimio isimame imara kupigania haki za Wakenya,” akaongeza Bw Musyoka.

Makamu huyo wa rais wa zamani alikuwa akizungumza katika soko la Kenyatta eneobunge la Lang’ata, Nairobi saa chache baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la Nairobi Baptist.

Alisema mkutano kati ya vigogo wa Azimio baada ya Bw Odinga kutangaza tamanio lake ni ishara kuwa hakuna utengano wala hapafai kuwapo hofu kwamba siasa za upinzani zitasambaratika bila uwepo wa kiongozi huyo wa ODM.

“Ninawahakikishia kuwa hakuna pengo na kile kilichotokea kwa Raila Odinga ni kitu tunachojivunia. Tutatampigia kampeni apate cheo cha AU kwa sababu sasa yuko juu ya siasa za nchi,” akaongeza Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alikuwa ameandamana na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, mwenzake wa Kitui Enock Wambua, wabunge Musili Mawathe (Embakasi Kusini), Stephen Mule (Matungulu), Edith Nyenze (Kitui Magharibi) miongoni mwa wanasiasa wengine.

Akionekana kuwa kifua mbele katika kivumbi vha kurithi uongozi wa siasa za upinzani bila uwepo wa Raila, Bw Musyoka aliashiria kuanza maandalizi ya siasa za uchaguzi mkuu wa 2027.

Alisema kuwa utata wote ambao uligubika uchaguzi wa 2022 lazima ushughulikiwe kupitia Ripoti ya Maridhiano (NADCO) ambayo inatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa baada ya Bunge kurejelea vikao vyake wiki jana.

“Hakuna haja ya kuelekea katika uchaguzi wa 2027 kama masuala tata ya 2022 hayajasuluhishwa. Hayo yatafanyika iwapo yaliyomo kwenye ripoti ya Nadco yatatekelezwa,” akasema.

Bw Sifuna alisema kuwa iwapo Bw Musyoka ataendelea kushirikiana na Raila, basi watamuunga kinara huyo wa Wiper 2027.

“Hawa watu ni wafuasi wa Raila na mradi tu mnashirikiana, usiwe na wasiwasi. Kile Raila anasema ndio watafuata hata kama hayuko kwa siasa za Kenya,” akasema Katibu huyo wa ODM.

Bw Mawathe na Mule walisema kuwa Kalonzo anatosha kwa sababu amemuunga mkono Raila kwenye uchaguzi wa 2013, 2017 na 2022.

“Hata Raila akienda AU au New York, bado atakuwa kiongozi wetu. Kalonzo na Raila wamekuwa pamoja na bado 2027 Kalonzo anampeleka Zakayo (Rais Ruto) nyumbani,” akasema Bw Mawathe.

Bw Mule naye alidai kuwa Rais ana nia ya kuongoza Kenya kidikteta bila uwepo wa Raila.