Habari MsetoSiasa

Tuliamka asubuhi kukuchagua lakini umetusaliti, Waititu azomewa Githurai

June 2nd, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu Jumapili alikabiliwa na kibarua kigumu kusalimu umma uliomkemea vikali Githurai 45 katika ziara ya Naibu wa Rais William Ruto eneo hilo.

Dkt Ruto alikuwa amezuru eneo la Ruiru kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo na alikuwa ameandamana na baadhi ya wabunge kutoka kaunti ya Kiambu.

Lililoanza kama mzaha watu kukataa Waititu apokezwe mikrofoni kuwazungumzia Dkt Ruto alipomkaribisha, liligeuka kuwa ukumbi wa kumrushia maneno mazito.

Umati wa watu waliojitokeza ulionekana kutofurahishwa na gavana huyo, wakidai ‘ametuangusha’. “Umetusaliti, umetuangusha na vile tuliamka asubuhi na mapema siku ya kura kukuchagua,” walimzoea.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, Bw Waititu ambaye aliwania ugavana Kiambu kwa chama tawala cha Jubilee alimrambisha sakafu William Kabogo aliyetetea kuhifadhi kiti chake kama mgombea wa kujigemea, kwa idadi kubwa ya kura.

Waititu alizoa kura 353,604 naye Bw Kabogo akipata 69,916. Eneo bunge la Ruiru linalojumuisha Githurai 45 iliyoko wadi ya Mwiki, gavana Waititu alipata idadi kubwa ya kura.

Wakazi wa Githurai katika tukio la kuonesha ghadhabu zao kwa utawala wa Waititu, Naibu wa Rais Ruto alilazimika kuwatuliza akiwarai gavana atarekebisha. “Baba Yao (jina la lakabu la Waititu) ameskia na amejua makosa yake, atayarekebisha,” alisema DkT Ruto.

Mwezi uliopita, gavana Waititu alikuwa amekamatwa na makachero wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kwa ushirikiano na idara ya upelelezi wa jinai (DCI) kwa madai ya ubadhirifu wa fedha Kiambu.