Tulianza vibaya lakini tuna matumaini tutamaliza vyema – Mutuini Rangers

Tulianza vibaya lakini tuna matumaini tutamaliza vyema – Mutuini Rangers

Na JOHN KIMWERE

TIMU nyingi huanzishwa kwa makusudio tofauti ikiwamo kukuza wanasoka chipukizi kufuzu kushiriki soka la kimataifa miaka ya baadaye. Aidha waanzilishi wengi hupania kutumia uongozi na ujuzi wao kuhakikisha timu zao zinafanikiwa kushiriki soka la Ligi Kuu, amesema kocha wa Mutuini Rangers, Joseph Njau.

Mutuini Rangers ni miongoni mwa klabu kongwe nchini lakini haijawahi fanikiwa kushiriki ligi za juu nchini. Timu hii iliasisiwa takribani miaka 50 iliyopita lakini ukosefu wa udhamini umechangia kutopata fursa ya kuonesha ujuzi wake katika mchezo wa soka nchini.

”Ingawa nimetwaa mikoba ya kuongoza klabu hiii mwaka mmoja uliyopita ninafahamu bayana ukosefu wa ufadhili huchangia timu nyingi kutofanya vizuri kwenye ligi,” anasema na kuongeza kuwa matatizo ya kifedha yanadidimiza juhudi za kikosi chake kwenye kampeni za kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu. Ndio mwanzo klabu hiyo inashiriki ngarambe ya NWRL baada ya kupandishwa ngazi kwa kufanya vizuri kwenye kampeni za Ligi ya Kaunti msimu uliyopita.

”Ingawa tulianza kampeni zetu vibaya ninaamini wachezaji wangu wana uwezo wa kufanya kweli. Katika mpango mzima licha ya pandashuka tunazopitia tunalenga kujituma kiume tuhakikishe tunamaliza kati ya nafasi tano bora,” akasema.

Mutuini Rangers imepangwa Kundi A linalojumuishaa jumla ya timu 14. Anasema kuwa wapinzani wao wameanza mechi zao kwa kasi mno hali inayotisha timu zinazoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza.

Timu ya AFC Leopards Youth

Kocha huyo anasema wanakabiliwa na kibarua kizito mbele ya wapinzani wao kama KSG Ogopa FC, Shalom Yassets, Kuwinda United, Uweza Kabiria, Karura Greens, WYSA United na KYSA Karengata kati ya zingine.

”Hata hivyo natoa wito kwa wachezaji wangu kamwe wasilaze damu dimbani soka halina mkubwa na mndogo sio ajabu timu ndogo kushindwa timu kubwa.

Jambo lingine nawataka wachezaji wangu wamakinike zaidi kwenye mechi zetu wakifahamu hatuna la ziada tumepania kumaliza kati ya nafasi bora katika jedwali endapo hatutafanikiwa kuibuka mabingwa na kusonga mbele.”

Klabu hiyo inajivunia kunoa makucha ya wachezaji wengi na kufaulu kuchezea timu za ligi za juu akiwamo Fredrick Njoroge ambaye husakatia Kahawa United ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi inajivunia kushiriki mashindano mbali mbali na kushinda mataji mengi tu ikiwamo Fallen Heroes Memorial kati ya mengine.

Mutuini Rangers inajumuisha wachana nyavu kama Geofrey Kariuki, Daniel Mwangi, Michael Mubinu (naibu wa nahodha), Elly Kinyanjui, James Nyaga (nahodha), Collins Kamau, Samson Mungai, Austine Gitau, Mwaura wanjiku, Peterson Paul, George Muchene, John Chege, Benard Kimani, James Mungai, James Gacheru na James Kirima.

You can share this post!

Mtambue ‘Kanini’ wa kipindi cha Maria

ANGELA CHEGE: Analenga kumpiku Anne Kansiime