HabariSiasa

Tulieni, mazuri yako njiani – Raila

August 20th, 2018 2 min read

Na PATRICK LANG’AT

KIONGOZI wa Upinzani, Raila Odinga Jumapili aliwaomba wafuasi wake kuwa na subira kuhusu manufaa ya muafaka wa kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Wafuasi hao wamekuwa wakishinikiza kujumuishwa kwake serikalini, baada ya viongozi hao kutangaza kusitisha uhasama kati yao na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo.

Lakini Bw Odinga aliwaahidi kungoja akisema hatimaye “watapata manufaa.”

Bw Odinga alisema kuwa safari ya kuelekea “Kanani” ingalipo, akiahidi italeta manufaa makubwa kwao.

“Nimesikia watu wakisema kwamba wanataka matokeo halisi ya “Kanani.” Hilo ni sawa, lakini lazima kwanza tumalize mchakato wa kujenga daraja, ndipo tuvuke Mto Jordani hadi Kanani. Huko, tutapata maziwa na nyama,” akasema, alipohutubu katika Kanisa la Friends Quakers Maringo, jijini Nairobi.

Bw Odinga alionekana kumjibu mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang, aliyemwomba kuwafafanulia kuhusu “manufaa ya muafaka huo.”

“Nafahamu kwamba mnaandaa mambo mazuri na Rais Kenyatta. Ninakuomba mharakishe maandalizi yake, ili tusipoteze imani. Tunapaswa kufahamu kuhusu masuala hayo sasa,” akasema Bw Kajwang.’

Kufuatia muafaka huo, kumekuwa na maswali kutoka kwa wafuasi wa Bw Odinga kuhusu manufaa watakayopata kutokana na muafaka huo.

“Ikiwa ni mapinduzi tunayoandaa, basi mambo yatafanyika haraka. Lakini haya si mapinduzi, bali ni mchakato wa kurejesja uthabiti wa kisiasa nchini,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na kituo kimoja mapema mwezi huu.

Bw Odinga alizungumza wakati kumekuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa Kundi la Kutekeleza Makubaliano hayo, baada ya kuibuka kwamba kundi hilo linakabiliwa na ukosefu wa fedha. Kundi hilo linaongozwa na Seneta wa Garissa, Yusuf Haji.

Hazina ya Kitaifa imedaiwa kuchelea kutoa Sh350 milioni ambazo kundi hilo lilikuwa likiitisha ili kutekeleza mpango huo.

Hata hivyo, Bw Odinga hakuzungumzia lolote kuhusu ripoti hiyo, ila alisifia muafaka huo kuwa “mwokozi wa mustakabali wa kisiasa Kenya.”

Akirejelea hadithi ya Biblia kuhusu wanawake wawili ambao waling’ang’ania mtoto mbele ya Mfalme Solomoni, ambapo mmoja alimtaka akatwe, Bw Odinga alisema muafaka huo ulifikiwa kwa kuwa “Kenya ni kubwa kuliko kila mtu.”

“Nilisema ninampenda mtoto huyu aitwaye Kenya sana, hivyo tunapaswa kumuacha aishi. Hatupaswi kumkatakata,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa licha ya uhuru wa kikatiba uliopo, tume za kikatiba zilizopo hazijakuwa zikifanya kazi ifaavyo.

Bw Odinga alifikia muafaka huo na Rais Kenyatta kama njia moja ya kutuliza taharuki ya kisiasa ambayo iliikumba nchi kufuatia uchaguzi tata wa Oktoba 26 mwaka uliopita.

Miongoni mwa masuala makuu yaliyojumuishwa kutatuliwa ni mchakato wa kutathmini asasi za uchaguzi, hasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hii ni kutokana na madai ya tume hiyo kutowajibika kwenye uchaguzi wa urais wa Agosti 8, ambao ulipelekea Mahakama ya Juu kuufutilia mbali.