Michezo

Tulieni mtatuzwa pesa, Mung’aro aambia washindi wa Governor’s Cup

May 17th, 2024 3 min read

NA MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kilifi Gideon Mung’aro amewataka washindi wa vitengo mbalimbali vya kipute cha soka kinachofadhiliwa na serikali ya kaunti hiyo watulie watatuzwa pesa.

Hii ni baada ya mabingwa kutishia kuandamana baada ya Wizara ya Michezo ya Kilifi kushindwa kukamilisha ahadi yake ya kupeana zawadi ya pesa wiki jana.

Akiwa Magarini, Gavana Mung’aro katika kikao na wananchi, aliahidi kufuatilia fedha hizo.

“Wakati kipute cha Governor’s Cup kiliandaliwa, pesa zilitengwa na itabidi mimi mwenyewe nifuatilie ili washindi wapate haki yao,” akasema gavana Mung’aro.

Licha ya kutangaza kwamba mabingwa wa Kilifi Governors Cup katika viwango vya kaunti, maeneobunge na wadi wangeponyoka na zawadi za pesa, ahadi hiyo imebaki kuwa ahadi hewa.

Wizara hiyo ikisalia kimya, mabingwa wa mashindano hayo wamekosa kufahamu hatima ya zawadi hizo, mwezi mmoja baada ya mashindano hayo kukamilika rasmi.

Kwa sasa timu zote zinazodai pesa hizo zimetishia kuandaa maandamano hadi kwa Ofisi ya Gavana wa Kaunti ya Kilifi ili kuwasilisha malalamishi yao.

Akizungumza kwa niaba ya timu ya Sabaki iliyocheza fainali za mashindano ya Governor’s Cup na kuibuka ya pili katika kaunti nzima, nahodha wa timu hiyo, Masha Kazungu, alieleza kuwa hakujakuwa na taarifa kamili kuhusu zawadi hizo, licha ya kuahidiwa kukabidhiwa “bila kuchekewa”.

“Tulipata habari kuwa tungepewa pesa zetu wiki jana na pia tungekuwa na mkutano Jumatatu hiyo baadaye wanatupigia simu kutueleza kuwa waziri hayuko ameenda mazishini,” akasema Kazungu.

Kazungu alielezea masikitiko yake na kusema kuwa wako gizani wasijue linaloendelea.

“Kipute cha Governor’s Cup kilipoanza, tuliambiwa kuwa washindi wangepewa pesa siku ya fainali lakini sasa hatuelewi huu mchezo unaoendelea kwa sasa,” akasema.

Wachezaji wa timu hizo wakiongozwa na Elias Mugendi, ambaye ni naibu nahodha wa Junju iliyoibuka mabingwa wa Kilifi Governor’s Cup, wameitaka wizara ya michezo kaunti ya Kilifi kuwa wazi.

Wanadai mikutano inayosemekana kuandaliwa na wizara hiyo imakosa kufanyika kila mara.

“Tunaomba wahusika wawe na uwazi kwa kila jambao wanlofanya kwa sababu tulipoteza muda wetu na nguvu zetu halafu kufikia sasa wanatuahidi wakati ligi hii ilitengewa pesa wakati tulipewa tu mabango ya cheki. Hatujui wanaficha nini kama hakuna pesa zilifunjwa watuambie pia,” akasema Mugendi.

Meneja wa timu ya Sabaki Bw Nelson Katana, alisema kuwa kutokana na sintofahamu hiyo, timu husika zimeanza harakati za kuandaa maandamano ili kuhakikisha zawadi hizo zinawafikia walengwa.

“Itabidi watu waandamane iwapo hizo peza hazitatoka kwa sababu washindi wanasubiri kufahamishwa yanayoendelewa lakini hadi hadi sasa timu katika hizo wadi zote hakuna kitu wamepata,” akasema Bw Katana.

Mipango hiyo ya maandamano inajiri juma moja baada ya maswali mengi kuibuka yakielekezwa katika Wizara ya Michezo kaunti ya Kilifi kutokana na zawadi za mabingwa wa mashindano hayo.

Waziri wa Michezo Kaunti ya Kilifi Dkt Dama Masha alisema idara yake imepanga mkutano na washindi wa wadi, maeneobunge na mabingwa wa mashindano hayo ili kuzungumzia jinsi ya kuboresha mashindano hayo katika siku zijazo pamoja na pesa za washindi hao.

Alipuuzilia tetesi kuwa pesa hizo hazipo na kusema washindi hao watapokea pesa zao kutoka kwa serikali, zawadi hizo zikiwa jumla ya zaidi ya Sh3milioni.

“Kuna wengine wanadhani pesa zilienda na MCAs na huo ni uongo, wengine wanasema tunadanganywa, Idara hii ya michezo inapenda kupanga vitu vyake na imepanga kwa uwazi pesa zitalowa ndani ya wiki hii,” akasema.

Hata hivyo ilibainika kuwa mameneja na makocha wa timu zinazodai zawadi zao hawajajulishwa kuhusu mkutano huo, taarifa zikieleza kuwa mkutano uliopangwa unahusisha maafisa wa idara ya michezo pekee.

Kocha wa timu ya Kararacha Bw Richard Charo alieleza kuwa kufikia sasa, hawajui mustakabali wa zawadi zao za pesa licha ya kukabidhiwa vikombe pekee.

Washindi wa wadi walitarajiwa kupata Sh50,000 na wa maeneobunge Sh100,000.

Mshindi wa fainali alitarajiwa kupata Sh500,000 naye wa pili na wa tatu Sh300,000 na Sh200,000 mtawalia.

Bw Mung’aro alidai huenda pesa hizo zikatoka mwishoni mwa wiki hii.

Gavana Mung’aro alizindua rasmi ligi hiyo Oktoba 2023 katika uwanja wa Kibaokiche katika eneobunge la Kaloleni.

Ligi hiyo ilitarajiwa kukamilika Desemba 12, 2023, lakini ilisitishwa kwa muda kufuatia madai ya ufisadi, jambo ambalo lilifanya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) na Mamlaka ya Kudhibiti Uagizaji Huduma na Bidhaa katika Sekta ya Umma (PPRA) kuingilia kati na kuanzisha uchunguzi.

Ligi hiyo iliyendelea na kukamilika rasmi mnamo Aprili 15, 2024.

[email protected]