Habari Mseto

Tuliiona ndege ikichomeka ikiwa angani – Mashahidi

March 12th, 2019 2 min read

VALENTINE OBARA Na MASHIRIKA

UCHUNGUZI wa kujua chanzo cha ajali ya ndege iliyotokea Jumapili na kusababisha vifo vya watu 157, wakiwemo Wakenya 32 nchini Ethiopia, umeshika kasi baada ya chombo muhimu cha ndege hiyo kupatikana.

Hayo yalijiri huku wachunguzi wakitathmini kuhusu uwezekano kwamba ndege iliangushwa, ikizingatiwa Serikali ya Amerika ilikuwa imeonya raia wake Ijumaa kutosafiri katika uwanja wa ndege wa Bole nchini Ethiopia mnamo Jumapili.

“Raia wa Amerika wameshauriwa wasiwasili wala kusafiri katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Bole, Machi 10, na wafanyakazi wa ubalozi pia wamekatazwa kwa muda kutosafiri kuelekea Oromia,” ilani hiyo ikasema.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la Oromia, ambako kumekuwa na maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia. Hata hivyo, wataalamu walisema ukweli utajulikana baada ya upelelezi kukamilika.

Maafisa walipata kifaa cha kurekodi shughuli za ndege almaarufu kama ‘black box’ kutoka kwenye vifusi vya ndege ya shirika la Ethiopian Airlines, aina ya Boeing 737 MAX 8 huku uvumi ukienea kuhusu chanzo cha ajali.

Kwa kawaida, wapelelezi wa ajali za ndege huchunguza masuala kama vile ubora ndege, weledi wa marubani, hali ya hewa na uwezekano kwamba ndege iliangushwa kusudi pengine na magaidi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Ethiopian Airlines, Tewolde GebreMariam alipohojiwa Jumapili alisema hawatapuuza uwezekano wa ugaidi katika uchunguzi utakaofanywa.

Mbali na maafisa wa Serikali ya Ethiopia, upelelezi huo unashirikisha wapelelezi wa Serikali za Kenya na Amerika na wataalamu wa ndege kutoka kampuni ya Boeing iliyo Amerika.

Walioshuhudia kisa hicho katika eneo la Bishoftu, kilomita 60 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bole, ambapo ndege nambari ET302 ilikuwa imetoka, walisema ilianza kuwaka moto ikiwa angani.

“Ndege hiyo ilikuwa tayari imeshika moto kabla ya kuanguka. Ilipoanguka kulikuwa na mlipuko mkubwa. Moto ulikuwa umewaka katika upande wa nyuma na ndege ilikuwa ikiyumbayumba kwa kishindo,” akasema shahidi Tegegn Dechasa, aliyehojiwa katika eneo la mkasa.

Shahidi mwingine, Sisay Gemechu alisema: “Ilionekana rubani alilenga kutua kwenye uwanja tambarare ulio hapa karibu lakini ndege ikaanguka kabla ifike hapo.”

Waziri wa Uchukuzi, James Macharia alisema Kenya imetuma mpelelezi wake Ethiopia kwa vile ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya raia walioaga.