Tuliteua Bi Kavindu kwa misingi ya sifa za uongozi – Kalonzo

Tuliteua Bi Kavindu kwa misingi ya sifa za uongozi – Kalonzo

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amefafanua kuwa chama hicho hakijaongozwa na nia ya kuvunja familia kwa Bi Agnes Kavindu Muthama kama mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos.

Akiongea alipompokeza rasmi Bi Kavindu cheti cha kuwania kiti hicho katika uchaguzi huo wa Machi 18, Bw Musyoka alisema kuwa Wiper ilizingatia tajriba na sifa za uongozi wa mwanasiasa huyo wala sio uhusiano wake wa kifamilia.

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta wa Machakos Boniface Mutinda Kabaka.Bi Kavindu ni mke, aliyetengana, wa Seneta wa zamani wa Machakos Johnson Muthama ambaye ndiye mshirika mkuu wa Naibu Rais William Ruto kutoka eneo la Ukambani.

Bw Muthama ambaye ni kiongozi wa chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA), ametangaza kuwa chama hicho kitadhamini mgombeaji katika uchaguzi huo mdogo.

“Tumemteua Bi Kavindu kwa sababu ni kiongozi mwenye sifa zinazolandama na sera zetu kama chama cha Wiper. Ni kiongozi mwadilifu ndio maana Rais Uhuru Kenyatta alimteua kama mwanachama wa Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) na mwanachama wa Bodi ya Kampuni ya Maji ya Tana Athi. Hatukuongozwa na nia ya kuvuruga familia ya rafiki yetu wa zamani,” Bw Musyoka akawaambia wanahabari katika makao ya Wiper, Karen, Nairobi.

Mgombeaji wa Wiper katika uchaguzi mdogo wa wadi wa Kitise/Kithuke, Makueni Sebastian Muli Munguti pia alikabidhiwa cheti cha uteuzi na mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya Wiper Bi Agatha Solitei.

Bi Kavindu alipata idhini ya kupeperusha bendera ya Wiper katika uchaguzi huo mdogo wa useneta baada ya watu wengine waliotaka tiketi hiyo kujiondoa na kuapa kumuunga mkono.

Wao ni aliyekuwa Mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile, Mshirikishi wa kampeni za BBI Ukambani Jackson Kala na mjane wa marehemu Kabaka Bi Jeniffer Mutinda.

Bw Musyoka ambaye pia Balozi wa Serikali katika Mpango wa Amani nchini Sudan Kusini, alitumia jukwaa hilo kumshambulia Dkt Ruto kwa kupinga wazo la Rais Uhuru Kenyatta kuhusu urais wa mzunguko.

Bw Musyoka alidai kuwa Dkt Ruto alitumia asilimia 50 ya usemi aliyopewa katika serikali ya muungano wa Jubilee mnamo 2013 kuteua watu kutoka jamii yake pekee, tofauti na Rais Kenyatta.

Bi Kavindu ambaye aliwania kiti cha Mwakilishi wa Wanawake Machakos kwa tiketi ya Jubilee katika uchaguzi wa 2017 alisema kuwa alihamia Wiper kwa idhini ya Rais Kenyatta.

Tayari Chama cha Maendeleo Chap Chap (CCM), chake Gavana Alfred Mutua, kimemteua aliyekuwa Waziri wa Maji na Mbunge wa Mwala Mutua Katuku, kuwa mgombeaji wake. Nacho chama cha UDA kinapania kuteua aliyekuwa Naibu Gavana wa Machakos Benard Kiala.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Uhuru, Ruto wajue dunia nzima inawatazama

Serikali yaonya wasimamizi wa vyama vya kahawa