Habari

Tulivyolinda 'bedroom' ya baba

November 9th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa chama cha ODM, wamefichua kuwa walitumia mbinu ili kuhakikisha kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra ameibuka mshindi.

Ijumaa, maafisa wa chama hicho walikiri kwamba walikuwa na kituo cha kujumlisha matokeo baada ya kuhesabiwa vituoni ili kuzima wizi wa kura.

Wakizungumza baada ya Bw Benard Okoth Imran kutangazwa mbunge mteule wa eneobunge hilo, viongozi hao walisema hawakutaka kumuaibisha kiongozi wa chama chao Raila Odinga ambaye alitangaza eneo hilo kuwa chumba chake cha kulala kisiasa.

“Mara hii tulijipanga na kulinda kura zetu kwa njia zote. Lakini kando na hilo, mpinzani wa Jubilee hakuwa chochote akilinganishwa na Bw Imran. Huwezi kuchokoza Bw Odinga Kibra na utarajie kwamba utashinda huku wafuasi wake wakiwa wamenyamaza tu,”alisema mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi na kuongeza, “Sisi hatukutumia ghasia dhidi yao jinsi wanavyodai bali mara hii raia ndio walijitokeza kukomesha ufidhuli wao wa kutusi Bw Odinga kila walipofanya mikutano maeneo mengine ya nchi.”

Bw Mbadi alisema walikuwa na kituo chao cha kujumuisha matokeo katika afisi za wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga na kwa kweli matokeo waliyopata yalitofautiana kidogo tu na yale yaliyotolewa na IEBC.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM aliye kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa na mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, walisema hawangeruhusu Dkt Ruto na wabunge wa Jubilee kuteka eneobunge hilo kisiasa.

“Huwezi kuja Kibra na upimane nguvu na baba. Sasa tuna ufunguo wa chumba cha kulala na tumewaonyesha kivumbi kwa kupata ushindi mkubwa. Wao ni waoga na sasa wametawanyika wote,” alisema Bw Mohamed katika kituo cha kujumuisha kura cha Chuo cha Mafunzo cha Nairobi City Inspectorate.

Uchaguzi huo ulikuwa umetajwa kama kinyang’anyiro kati ya Bw Odinga na Bw Ruto kuonyesha ubabe wa kisiasa.

Hata hivyo, Dkt Ruto alilemewa sana na mbinu za ODM kwenye uchaguzi huo kiasi kwamba, mgombeaji wa Jubilee Macdonald Mariga alikubali kushindwa mapema baada ya kura kutoka kwa vituo 61 pekee kati ya vituo 183 kuhesabiwa.

ODM iliendesha kampeni kali yenye propaganda Kibra viongozi wake wakitoa matamshi makali dhidi ya Dkt Ruto na Bw Mariga.

Chama hicho kiliwarai wanasiasa wenye ushawishi kutoka jamii zinazoishi Kibra ili kumpigia debe Bw Okoth wakiwemo wa chama cha Jubilee wakimtaja kama mgombeaji wa handisheki.

Mbinu yazaa matunda

Mbinu hii ilizaa matunda Bw Okoth aliposhinda kwa kura, 24,636 dhidi ya 11,230 za Bw Mariga. Eliud Owalo wa chama cha Amani National Congress cha Musalia Mudavadi alikuwa wa tatu kwa kura 5,275.

Viongozi mbalimbali walimpongeza Okoth kufuatia ushindi huo wakisema ulionyesha handisheki inazaa matunda.

“Asante nyote wafuasi wa ODM katika eneobunge la Kibra kwa kudhihirisha kweli ninyi ni wanademokrasia. Asanteni kwa uvumilivu wenu na kwa kupiga kura licha ya changamoto mliokumbana nazo. Pongezi ndugu Imra Okoth kwa ushindi wako mtamu,” akasema kupitia akaunti yake ya Twitter.

“Ushindi wako ni thibitisho kuwa Kibra inaweza kuamua. Ni ishara kwamba Handisheki ya UhuRao haiwezi kutikiswa. Sasa BBI Kenya twende kazi, Mbele Pamoja. Kibra ni ODM, Kibra ni kwetu Uhuru akiwa na Baba. Kenya mpya inaundwa,” alisema aliyekuwa mbunge wa Mukurweni Kabando wa Kabando.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru aliyempigia debe Bw Okoth alisema: “Pongezi Mbunge Mteule wa Kibra (Imran) na watu wa Kibra kwa kumpigia kura mwana halisi wa Kibra.

“Asante kwa handisheki. Walituchekelea mbeleni lakini hii ni ithibati kwamba mambo yamebadilika mashinani. Hongera handisheki na sasa tunasubiri ripoti ya BBI,” Bi Waiguru akaongeza.

 

Na CECIL ODONGO, BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA