Michezo

Tulizeni boli, mabinti wa Mathare waambia wenzao wa Zetech

September 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MATHARE United Women (MUW FC) ilitoka chini kwa kulazwa mabao 2-0 na kubahatika kulazimisha sare ya magoli 2-2 dhidi ya Zetech Sparks (Soccer Queens) kwenye mechi ya Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) iliyopigiwa uwanja wa MYSA Komarocks, Nairobi.

Zetech chini ya nahodha, Puren Anyetu ilianza mchezo huo kwa kasi huku ikitafuta mabao ya mapema. Juhudi za vipusa hao zilifaulu kupata matunda mema dakika ya 20 pale Lydia Akoth alipowatingia bao la kwanza.

Goli hilo lilionekana kuchochea wapinzani wao lakini wapi jitihada zao ziliambulia patupu. Dakika kumi baadaye Zetech ya kocha, Bernard Kitolo ilijiongezea bao la pili lililofunikwa kimiani na Puren Anyetu.

Kipindi cha lala salama, MUW FC ilirejea dimbani kivingine ikilenga kuzinduka na kubadilisha matokeo hayo. Kocha wake, Mary Odhiambo alifanya mabadiliko katika kikosi hicho alipomvuta nje, Mercy Mwende huku Stacy Adhiambo alijaza nafasi yake.

Nguvu mpya aliofanikiwa kuchochea wenzake na kubadilisha mchezo huo huku wakifanya wapinzani wao kukosa ujanja.

Mathare ilipata bao la kwanza kupitia juhudi zake Diana Wacera alipotuma kombora nzito iliyomgonga Consolata Wanjiku wa Zetech hadi wavuni. Wachana nyavu hao waliendelea kupigana kwa udi na uvumba kabla ya Judith Atieno kusawazisha bao la usiku kunako dakika ya tisini.

”Kusema kweli soka haina heshima. Tulianza mchezo wetu vizuri lakini ndani ya kipindi cha pili tulipoteza mwelekeo pia ushirikiano mzuri jambo lililotugharimu kuyeyusha alama mbili muhimu,” alisema nahodha huyo wa Zetech Sparks. Hata hivyo aliongeza kuwa wanahitaji kushiriki mazoezi makali ili kujiweka fiti kukabili wapinzani wao kwenye mechi zilizosalia.

Ufanisi wa pointi moja uliibeba Mathare na kurukia afasi ya 12 kwa kuzoa alama 15, moja mbele ya Nyuki Starlets iliyofurushwa katika kipute hicho baada ya kukosa kushiriki mechi tatu za ugenini mfululizo.